Na Miraji Msala
Wakazi wa Goba, Msumi, Tegeta A na maeneo jirani wanaendelea kunufaika na kasi ya ujenzi wa barabara muhimu zinazounganisha maeneo hayo, chini ya usimamizi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA). Ujenzi wa barabara za Wakorea–Goba, Msumi na Goba–Mkorea unaotekelezwa kwa kiwango cha lami umeibua matumaini mapya kwa wakazi baada ya miaka mingi ya changamoto za usafiri.
Meneja wa TARURA mkoa wa Dar es Salaam, Geofrey Mkinga, amesema ujenzi wa barabara ya Wakorea–Goba yenye kilometa 9.9 umefikia hatua nzuri na unatarajiwa kukamilika Agosti mwaka huu.
Tulianza mwezi wa tano na tunamaliza mwezi wa nane. Itatoa ahueni kubwa kwa wakazi wa maeneo haya,” alisema.
Sambamba na hilo, ujenzi wa daraja la Tegeta A Mpakani unaendelea kwa lengo la kulifanya lipitike wakati wote, hasa msimu wa mvua ambao kwa miaka mingi limekuwa likijaa maji na kukwamisha shughuli za wananchi.
TARURA imesema inatekeleza mpango mpana wa kuboresha kilomita 750 za barabara katika jiji la Dar es Salaam, ambapo kilomita 259 tayari zimekamilika usanifu wake. Katika Manispaa ya Ubungo, barabara ya Goba–Mkorea inayojengwa na Zhongmei Group nayo inaendelea kwa kasi, huku Mhandisi wa mradi, Amani Alex, akibainisha kuwa kazi inafanyika kwa kuzingatia viwango na muda.
Barabara hizi zinatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha biashara katika maeneo ya Tegeta A, Msumi , kutokana na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, kupunguza muda wa kusafiri na kupunguza gharama za usafiri ambazo kwa sasa ni kubwa.
Kuna daladala moja tu. Tunaingia gharama ya zaidi ya shilingi elfu 2000 kwa bajaji,” alisema Janeth Mgaya wa Goba Mpakani, akionyesha matumaini kuwa hali hiyo itabadilika mara barabara zitakapokamilika.
Miradi ya Wakorea–Goba ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuboresha miundombinu ya barabara nchini kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kurahisisha huduma kwa wananchi. TARURA imeendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha inakamilika kwa ubora na ndani ya muda uliopangwa.
Kukamilika kwa barabara hizo kunatarajiwa kuondoa adha za usafiri kwa maelfu ya wakazi wa Goba, Msumi, Tegeta A na maeneo mengine jirani, na kuwa msingi wa kuongeza fursa za biashara, huduma na ustawi wa jamii.






No comments:
Post a Comment