HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 16, 2016

WAZIRI MBARAWA AITAKA SUMATRA KUDHIBITI AJALI

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa pili kulia) akitoa maelekezo kwa Meneja wa Kiwanja cha ndege cha Kikwetu Mkoani Lindi Bw. Boniface Njanda (Wa kwanza Kulia) wakati alipotembelea uwanja huo.

Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) mkoa wa Lindi Eng. Isaac Mwanawima akitoa taarifa ya utendaji wa Wakala huo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa kwanza kushoto) wakati alipotembelea wakala huo.



LINDI TANZANIA,Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameutaka uongozi wa  Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) kutoa adhabu kali kwa wamiliki wa vyombo vya usafirishaji na madereva wazembe wanaosababisha ajali za barabarani.

Ameyazungumza  hayo wakati  wa ukaguzi wa utendaji kazi kwa wafanyakazi wa taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo pamoja na miundondombinu ya Barabara, Bandari, Mawasiliano na kiwanja cha ndege cha Kikwetu mkoani Lindi. 

Profesa Mbarawa amesema kuwa ongezeko la ajali zinazosababisha vifo kutokana na uzembe wa madereva, kutofuata sheria na alama zinazowekwa  barabarani zizidhibitiwe ili kuokoa maisha ya watanzania na nguvu kazi ya Taifa. 

“Nataka kuona wamiliki wa vyombo vya usafiri na madereva wazembe wanaposabisha ajali na kuua watu wanafutiwa leseni zao vile vile nawataka mfikirie kwanini watanzania wengi wanaendelea kufa kwa ajali za barabarani ili muweze kutafuta ufumbuzi wa namna ya kudhibiti ajali hizo”, amesisitiza Prof. Mbarawa. 

Katika hatua nyingine Waziri Mbarawa amemuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Eng. George Sambali kukamilisha kazi ya kupima eneo la kiwanja cha Kikwetu ili kupata hati miliki na kudhibiti uvamizi wa kiwanja hicho.

“Kama kiwanja hiki hakitapimwa watu watavamia eneo la kiwanja na Serikali italazimika kuingia gharama za kulipa fidia hivyo kuchelewesha maendeleo ya uwanja huo”, amesema Prof. Mbarawa.

Ameongeza kuwa Serikali iko kwenye hatua za mwisho za kutafuta fedha kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ili kuimarisha miundombinu ya kiwanja hicho na  kuongeza chachu ya maendeleo Mkoani humo.

Naye Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Kikwetu, mkoani Lindi Bw. Boniface Njanda amemuhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa Mamlaka itafanya tathmini ya Kiwanja hicho kabla ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami.

Waziri Mbarawa yupo katika ziara ya kukagua utendaji kazi kwa wafanyakazi wa taasisi zilizopo chini ya Wizara na kuangalia maendeleo ya utekelezaji wa miradi katika kanda ya kusini.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments:

Post a Comment

Pages