Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais WA Zanzibar itahakikisha inatoa kila aina ya ushirikiano kwa uongozi wa wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira ya Tanzania ili kuweza kufanikisha kazi zake kwa maslahi mapana ya wananchi wa pande zote mbili za Muungano.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na Uongozi wa Wizara hio uliofika ofisini kwake vuga kwa lengo la kujitambulisha.
Mhe. Hemed amesema suala la Muungano ndio kiungo kikubwa cha nchi kwa wananchi wa pande zote mbili hivyo ni vyema kuhakikisha viongozi wake wanashirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha masuala yanayohusu Muungano yanatekelezwa ipasavyo kwa maslahi mapana ya Taifa la Tanzania.
Amesema Zanzibar kuna miradi mingi inayofadhiliwa na Serikalini ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia wadau mbali mbali hivyo amewataka viongozi hao kuhakikisha wanaelekeza nguvu zaidi katika suala la mazingira hasa katika maeneo ambayo yameathirika na maji ya bahari.
Makamu wa Pili wa Rais amesema katika kuulinda na kuuenzi Muungano kuna umuhimu wa kuendelea kutolewa elimu na kuielimisha jamii juu ya umuhimu na faida za muungano huo.
Sambamba na hayo amesema pande zote mbili za Serikali zitaendelea kuulinda, kuuenzi na kuudumisha Muungano ikiwa ni urithi wa vizazi vya sasa na vya baadae na kuendelea kuwaenzi waasisi wa Muungano Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhandisi Hamadi Yussuf Masauni ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa maendeleo makubwa yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miaka mitano 5 ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Nane ( 8 ) ikiwemo; Uimarishaji wa huduma za jamii (maji na hospitali), ujenzi wa barabara na mambo mengine mengi.
Amesema katika miaka mitano iliyopita hoja nyingi za Muungano zimepatiwa ufumbuzi hivyo, Serikali zote mbili zitahakikisha hoja zilizobakia zinapatiwa ufumbuzi kwa maslahi mapana ya wananchi wa pande zote mbili.
Amesema Ofisi ya Rais Muungano na Mazingira ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukuza biashara ambapo Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania tayari ameridhia kuanzishwa kwa Idara ya Uchumi wa Buluu na kuahidi kuja kujifunza Zanzibar kutokana na kupiga hatua kubwa katika sekta hio.


No comments:
Post a Comment