HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 10, 2025

WATANZANIA WASHAURIWA KUENDELEZA UTAMADUNI WA MAZUNGUMZO: BUTIKU

 Na Mwandishi Wetu


WATANZANIA wameshauriwa kuendeleza utamaduni kutumia njia ya mazungumzo pale wanapokutana na changamoto za kisiasa, kijamii na kiuchumi.


Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa siku moja wa mashauriano ulioandaliwa kwa pamoja na MNF na Taasisi ya Amani Tanzania.



Butiku alisema Tanzania ni nchi yenye historia ya aina yake katika kutatua migogoro ya ndani na nje hivyo ni vema utamaduni huo ukaendelezwa.


"Ndugu zangu Watanzania taasisi ya MNF na Taasisi ya Amani Tanzania leo tumekutanisha wazee na viongozi wa dini hapa Dodoma kwa lengo moja la kujadili amani yetu, hasa kutokana na vuguvugu la vijana wetu ambao Oktoba 29 waliandamana na kusababishia vurugu, vifo, majeruhi na uharibifu wa mali za umma na sekta binafsi," alisema.


Butiku utamaduni wa muda mrefu wa Watanzania umejikita kwenye  mazungumzo, uvumilivu na maridhiano, akisisitiza kwamba taifa bado lina uwezo kamili wa kutatua changamoto zake bila kukimbilia matumizi ya nguvu.


Alisisitiza kuwa matukio kama machafuko ya Oktoba 29, 2025 hayapaswi kurudiwa kamwe. Akizungumza jijini Dodoma 


Mwenyekiti huyo alisema malalamiko yanayotolewa na vijana nchini kote ni ya msingi na yanastahili kushughulikiwa.

Hata hivyo, alionya kuwa hakuna kiwango cha kufadhaika kinachoweza kuhalalisha vurugu au uharibifu wa mali za umma. 


“Ni lazima tuaminiane ili kutatua changamoto tunazokabiliana nazo. Tuna uwezo wa kufanya mazungumzo; hatupaswi kuruhusu matukio kama haya kujirudia,” alisema, akithibitisha kwamba Watanzania hawajapoteza uwezo wao wa pamoja wa kuzungumza na kufikia mwafaka kuhusu masuala ya kitaifa.


Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Amani Tanzania, Askofu Amos Muhagachi alisema watashirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha amani ya nchi inadumu muda wote.


Askofu Muhagachi alisema mikakati yao ni kuona kila Mtanzania anaishi kwa amani na kupata haki zake kwa kujibu wa Katiba na Sheria za nchi.


Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano Tanzania Sheikh Alhad Musa Salum aliwahimiza Watanzania kuiruhusu Tume ya Uchunguzi kukamilisha kazi yake bila kuingiliwa, akibainisha kuwa matukio ya Oktoba yalionyesha kuwepo kwa nguvu za ndani na za nje zinazolenga kuvuruga utulivu. 


Kwa upande wake Sheikh wa Mkoa wa Arusha Shaban Simba alitoa raia kwa wazazi kulea vijana wao kwa kufuata misingi bora, ikiwemo dini, kwani kwa sasa duniani imehamia kwenye mitandao.


"Wazazi naomba nitumie nafasi hivi kuwaomba msikubali mitandao ya kijamii ndio iwalee watoto wetu, hii sio sawa, turejee kwenye dini na tamaduni zetu, bila hivyo hawa G-Zee hatuwezi kuwadhibiti, " alisema. 


Katibu Mkuu wa Kanisa la Orthodox la Urusi nchini Tanzania, Godfrey Nestory, aliiomba Serikali kutoa ratiba ya wazi kuhusu lini mchakato wa Katiba Mpya utaanza tena


Akiwasilisha maazimio ya mkutano huo, Katibu wa Jukwaa hilo, Dkt. Chirangi Masuto, alisema washiriki wamesikitishwa sana na matukio hayo na wamepeleka rambirambi kwa familia zote zilizoathirika. Wajumbe walipitisha maazimio manne muhimu yanayolenga kuimarisha amani ya kudumu.


Waliwataka wananchi wote kuwa watulivu wakati wakisubiri matokeo ya Tume Huru ya Uchunguzi iliyoanzishwa na Rais kubainisha chanzo cha machafuko ya Oktoba. 


Walisema ripoti hiyo itakuwa msingi wa kujadiliana namna ya kusonga mbele.

Mkutano huo pia uliitaka serikali kutoa taarifa kamili kuhusu idadi ya vifo, kiwango cha uharibifu wa mali, na kutoa rambirambi pamoja na msaada wa kitabibu na kisaikolojia kwa waathirika.

Kuhusu madai ya muda mrefu ya mabadiliko ya katiba, jukwaa lilipendekeza kuanzisha upya mchakato wa Katiba Mpya kwa njia huru, shirikishi na yenye ratiba ya wazi, itakayohitimishwa kwa kura ya maoni ya wananchi.


Washiriki pia walisisitiza uzalendo, haki na uwajibikaji kama nguzo muhimu za umoja wa kitaifa. Waliwataka viongozi wa ngazi zote kuweka maslahi ya taifa mbele, kuhakikisha uwazi katika usimamizi wa rasilimali za umma, na kuzingatia uwezekano wa kuwaachia huru watuhumiwa wa kisiasa huku wakiboresha mifumo ya udhibiti na uwajibikaji.


Kuhusu tetesi za maandamano yanayotarajiwa kufanyika tarehe 9 Desemba 2025, jukwaa liliwahimiza wadau wote kukumbatia mazungumzo na upatanishi. Wananchi walishauriwa kuepuka kauli au vitendo vinavyoweza kuchochea mvutano wa kisiasa, kidini au kikabila.


Katika maoni yao binafsi, viongozi wa dini walionya kuwa amani haiwezi kudumu mahali ambapo hakuna haki. Mchungaji Felix Msumari wa KKKT Tanga alisema, “Amani bila haki inawafanya watu waogope kusema ukweli.”



No comments:

Post a Comment

Pages