Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam
"Shughuli za uvuvi ni sayansi, ni jambo linalohitaji utaalam wa wanasayansi na shughuli nyeti katika usalama wa chakula katika dunia yetu, ndio maanda leo nimekuja kuzindua Kongamano lao la Siku tatu lengo kubwa ni kuhakikisha shughuli za uvuvi na ukuzaji viumbe maji zinafanyika kisayansi, kisasa, zinatumia nyezo za kisasa na ubunifu ili wavuvi wadogo waweze kunufaika na jasho lao" amesema Balozi Dkt. Bashiru.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Dkt. Ismael Kimirei amebainisha kuwa wataalam wakiwemo wanasayansi, watafiti, wasomi wa vyuo Vikuu, wadau wa uvuvi na ukuzaji viumbe maji kutoka Nchi 17 duniani watajadili taarifa mbalimbali za kisayansi na tafiti ili kuiwezesha sekta ya uchumi wa buluu kuwa endelevu na kuwa na mchango katika uchumi kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Katika hatua nyingine, Waziri Balozi Dkt. Bashiru,ameshuhudia utiaji saini wa makubaliano ya ujenzi wa meli 3 za Uvuvi wa Bahari Kuu kati ya serikali kupitia Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) ambapo amesema ujenzi wa meli hizo utasaidia kwenda kuvua samaki bahari pamoja na kuifanya Bandari ya Uvuvi Kilwa kuwa na tija.
Nae, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Meena ameongeza kuwa mpango wa serikali ni kuwa na meli sita kwa ajili ya uvuvi wa bahari kuu ambapo meli nne zitakuwa Tanzania Bara chini ya Usimamizi wa Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) na Meli mbili zitakuwa Zanzibar na kutoa rai kwa watekelezaji wa mradi kuzingatia muda na kwa ufanisi ili meli hizo zianze kufanya kazi.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ng'wasi Damas Kamani amefafanua kuwa katika kipindi cha miezi tisa tangu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru akabidhiwe kuiongoza wizara hiyo, kumekuwa na hatua nzuri na muhimu za kulifufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) ikiwa ni pamoja na hatua hii ya ujenzi wa meli kwa ajili ya Uvuvi wa Bahari Kuu.






No comments:
Post a Comment