Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAFANYABIASHARA na wajasiriamali wametakiwa kutumia teknolojia, kujenga ushirikiano na taasisi za kifedha na kuimarisha usimamizi wa mitaji ili kuongeza ushindani na kufikia masoko mapya ndani na nje ya nchi.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, wakati wa kufunga Jukwaa la Instapreneur lililoandaliwa na Benki ya CRDB, ambapo amesisitiza umuhimu wa kuwa na mikakati inayowezesha biashara kukua kwa uthabiti na kukabiliana na changamoto za soko.
Chalamila amesema mafanikio ya biashara hayaamuliwi na wingi wa fursa zinazofuatwa, bali uwezo wa mjasiriamali kuweka malengo, kufanya maamuzi sahihi na kusimamia rasilimali alizonazo kwa nidhamu.
Amesema wajasiriamali wanapaswa kujifunza kutokana na changamoto wanazokutana nazo na kuchagua kwa umakini washirika wa biashara, akieleza kuwa maamuzi yasiyo sahihi yanaweza kuathiri mtaji na mwelekeo wa biashara.
Aidha, amewataka kujenga uhusiano mzuri na taasisi za kifedha ili kurahisisha shughuli zao na kuweka msingi wa ukuaji endelevu.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Feruzi Korongo, amesema benki hiyo inaendelea kuimarisha mifumo ya kidijitali inayowawezesha wafanyabiashara kufanya miamala, kutunza kumbukumbu za fedha na kufuatilia mauzo kwa urahisi.
Korongo amesema huduma hizo zina lengo la kuwasaidia wajasiriamali kufanya maamuzi kwa kutumia taarifa sahihi za biashara zao, huku benki hiyo ikiimarisha huduma za ufadhili, malipo ya kimataifa na ushauri wa kifedha.
Ameongeza kuwa uwepo wa CRDB nchini Tanzania, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Dubai unatoa fursa za kujenga uhusiano wa kibiashara na kutafuta masoko mapya katika maeneo mbalimbali.
Amesema benki hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wa sekta binafsi kutoa mafunzo, kuwaunganisha wajasiriamali na masoko na kuboresha huduma za kifedha, hatua zinazolenga kuimarisha biashara na kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa.









No comments:
Post a Comment