HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 10, 2013

Wabunge wanahonga Waandishi, Spika Je?

Mvutano Bungeni
Na Bryceson Mathias

HIVI karibuni Spika Anne Makinda, akijibu maswali ya waandishi kuhusu vurugu zinazotokea Bungeni, na hasa kuporwa au kugeuzwa kwa hoja za upinzani, aliibuka na kauli tata akidai vyombo vya habari na waandishi wanahongwa na wabunge ili waandikwe vizuri.

Ingawa hakufafanua ni kwa namna gani wabunge wanatoa hongo licha ya kusema wanatoa kitu kidogo ili waandikwe vizuri, na alikana madai kuwa anawakandamiza wabunge wa   upinzani na kuwabeba wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walio upande wa Serikali.

Makinda ni miongoni mwa Wabunge, nadhani alitoa kauli hiyo akijisahau kuwa ni Mbunge, ambapo kwa kuwatuhumu wandishi na vyombo kuhongwa na wabunge bila kuwataja majina, alikuwa anajijumuisha kwenye Orodha ya wanaotoa Hongo, aliyoiita kitu kidogo.

Mmoja wa wabunge wa CCM kanda ya Kusini ambaye hakutaka jina litajwe kutokana na kukasirishwa na kauli ya Spika kuwaita wananavihonga vyombo vya habari na wandishi alisema, “Kama wabunge tunatoa hongo, naye ni Mbunge, basi anatoa pia“.

Mbunge wa machachari wa (CUF) ambaye mara nyingi huuliza maswali magumu alisema, Kauli ya Spika anatakiwa aifute mara moja, inaweza ikasababisha malumbano makali katika Bunge lijalo, ili Spika athibitishe kwa ushahidi.

Mbunge wa viti maalum (CCM) kanda ya ziwa alisema, kama Spika hataifuta kauli yake, amewdhalilisha Wabunge na Bunge, ukizingatia yeye ndiye huongoza kiti. Kama huwa hawakemei bungeni, akasema nje?, “Ninaangalia uwezekano wa kumshitaki!”

“Ni ukweli usiopingika, hata yeye tumekuwa tukimuona akiwakandamiza wapinzani kama wanavyodai wananchi, hatujawahi kusema anahongwa. Je na sisi tumtuhumu anahongwa na nani?”. Asipofuta kauli, naandaa hoja binafsi dhidi yake.

Ingawa Makinda alijisafisha ati hana upendeleo katika uendeshaji wa vikao vya Bunge kama anavyoshambuliwa na baadhi ya watu na kwamba lawama zinazoelekezwa kwake zinatokana na watu kuangalia upande mmoja, Mbunge huyo alisema, Huwezi kusema huli nyama wakati mchuzi unakunywa!

Aliongeza, hakuna mtu asiyejua umuhimu wa hoja ya kushuka kwa Elimu na Mustakabali wake kwa Umma, lakini kuna mambo ambayo kiti katika hoja hiyo kilifanya sivyo ndivyo, kwa jambo   ambalo dhahiri lina maslahi ya umma! Mbona hatukumtuhumu kama alivyotufanyia?

Makinda alitoka kuzungumza na Spika wa Korea Kusini, Kang Chang Hee, alipojinasifu, "Ndiyo najua mnapewa 'kitu kidogo' na hawa wanaoanzisha vurugu bungeni, lakini kusema Spika anapendelea hili siyo kweli hata kidogo," alisema Spika.

“Iwapo ningekuwa na kawaida ya kuwakandamiza wabunge wa upinzani kwa kiasi kinachosemwa, wengi wa wabunge wa upinzani wasingekuwapo bungeni.

“Mimi siwapendelei wabunge wa CCM, ningekuwa hivyo hawa wapinzani wasingekuwapo bungeni,” alisema Makinda muda mfupi baada ya kuzungumza na ujumbe wa Bunge la Korea Kusini uliomtembelea ofisini kwake.

Hata hivyo, mbali ya Makinda kusema wakati wa kuendesha vikao vya Bunge halitakiwi kuwa na itikadi za vyama na kwamba kufanya hivyo kunaweza kusababisha vurugu, baadhi ya wananchi waliohojiwa walidai, ‘Penye ukweli uongo hujitenga, Kiti cha Spika akiwemo Makinda kina upendeleo.

Hata kama Spika alijitetea hivyo, wananchi wamedai wabunge wa upinzani kwa nyakati tofauti walimtupia lawama za wazi hususani bungeni kwamba anawapendelea wabunge wa CCM.

Miongoni mwa mambo yaliyotajwa, amekuwa akilaumiwa kukalia zaidi ya taarifa 10 za ushahidi juu ya kauli za wabunge wa upinzani zilizowasilishwa kwake kwa muda wote bila kusema lolote. Miongoni mwa ushahidi huo, umo wa mawaziri kusema uongo bungeni.
 
Ni rai yangu kabla ya Makinda kuvinyoshea vyombo habari na wandishi kidole, ni vema akaangali vidole vitatu vinavyomuuliza. Je wewe!
 
 
0715933308

No comments:

Post a Comment

Pages