HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 03, 2026

Benki ya CRDB Yazindua Kampeni ya 'Benki Kimpango Wako' kwa Mwaka 2026, Yasherehekea Mafanikio ya Mwaka 2025

Baada ya mwaka wa 2025 kuwa na ufanisi mkubwa katika biashara, ambapo Benki ya CRDB ilipata faida ya zaidi ya shilingi trilioni 1.04, leo benki hiyo imezindua kampeni ya mwaka 2026 inayoitwa ‘Benki Kimpango Wako’.

Kampeni hii inalenga kuboresha huduma kwa wateja kwa kupunguza muda wa kukamilisha miamala na kuwapa wateja uwezo wa kujihudumia kwa urahisi kutoka mahali popote duniani, wakati wowote wanapotaka.

Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, aliwashukuru wateja, wawekezaji, wabia wa kimkakati, na wadau wote kwa imani waliyonayo kwa benki hiyo.


 

Alieleza kuwa mafanikio ya mwaka 2025 yamechangiwa na ushirikiano mzuri kutoka kwa wateja binafsi, wajasiriamali, mashirika na serikali.

Nsekela alisema, “Mwaka jana tumepata faida kubwa na tutaendelea na azma yetu ya kuboresha maisha ya Watanzania na uchumi wa taifa letu. Kampeni hii ni sehemu ya juhudi zetu za kutoa huduma bora na za uhakika kwa wateja wetu wote."

Mwaka 2025, Benki ya CRDB ilijivunia kupata faida ya shilingi trilioni 1.04 kabla ya kodi, sawa na ongezeko la asilimia 33, huku faida baada ya kodi ikiwa ni shilingi bilioni 725, ongezeko la asilimia 31 ikilinganishwa na mwaka 2024.

Benki ya CRDB pia ilionyesha ongezeko kubwa katika mizania yake, ambayo ilifikia shilingi trilioni 22.2, huku mikopo iliyopewa wateja ikifikia shilingi trilioni 13.7. Nsekela alisisitiza kwamba ukuaji huu unamaanisha uwezo mkubwa zaidi wa kufadhili miradi ya maendeleo, kusaidia kukuza biashara na kutoa ajira mpya.


Kampeni ya ‘Benki Kimpango Wako’ inajumuisha maboresho ya mfumo wa uendeshaji wa benki (core banking system) ambao ulizinduliwa mwaka jana, na ofisi ya uwakilishi iliyozinduliwa Dubai mwanzoni mwa mwaka huu. Benki ya CRDB pia inahakikisha huduma bora kwa wateja kupitia matawi, CRDB Wakala, SimBanking, na huduma za benki mtandao.

“Tunawakaribisha wateja wetu kutoka Tanzania, Burundi, DRC, na Dubai kutumia huduma zetu zinazotumika popote duniani,” alisisitiza Nsekela.


Benki ya CRDB inatambuliwa kama moja ya benki imara Afrika Mashariki, na inahudumia wateja zaidi ya milioni 4, kupitia matawi 260 na mtandao wa huduma mbadala zaidi ya 25,000. Kampeni hii ya mwaka 2026 inatekeleza azma ya benki hiyo katika kutoa huduma za kifedha rahisi, za haraka na zinazokubalika na mikakati ya kiuchumi ya wateja wake.






No comments:

Post a Comment

Pages