Na Bryceson Mathias
HIVI karibuni Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mtwara ilimfutia shtaka la kesi ya uchochezi iliyokuwa ikimkabili Mbunge wa Mtwara Mjini (CCM) Hasnein Murji (46) aliyepandishwa kizimbani Juni 10, mwaka huu na kufunguliwa kesi ya uchochezi.
Hatua hiyo ilikuja baada ya Wakili wa utetezi, Peter Kibatala kuiomba mahakama kuifuta kesi hiyo iliposomwa Julai 3, mwaka huu kwa madai hati ya mashtaka ni dhaifu kisheria na haionyeshi ni makosa yapi mtuhumiwa aliyatenda.
Kibatala aliieleza mahakama kuwa kifungu cha 129 na 132 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ni lazima mshtakiwa aelezwe mashtaka yake wazi wazi yanayomkabili, jambo linalopelekea baadhi ya wanasiasa wahoji akumulikaye mchana usiku atakuchoma?
Murji alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani akikabiliwa na kesi ya uchochezi anayodaiwa kuifanya Januari 19,mwaka huu katika eneo la Ligula mkoani humo Mtwara.
Hakimu Mkazi Mfawidhi Dynes Lyimo alifuta shtaka hilo na kumwachia mshtakiwa huru baada ya kesi hiyo kuahirishwa tangu Julai 3, mwaka huu.
Miongoni mwa waliohusishwa na kesi hiyo ni viongozi wa upinzani Katani Ahmed (33) na Saidi Kulaga (45) wa CUF waliokabiliwa na mashtaka matatu ya kula njama, kufanya uchochezi na kuamsha hisia mbaya kwa wakazi wa Jamhuri.
Murji alikabiliwa na tuhuma za uchochezi wa vurugu za kupinga kujengwa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara hadi jijini Dar es Salaam, zilizosababisha vifo vya watu watatu na wengine kadhaa kujeruhiwa Mei, 2013.
ni rai yetu kufahamu kama Mahakama imemfutia mashitaka Murji, Waliomshitaki wamemuonea? Mbali ya kumuonea, Murji na wananchi wake wanakitazamaje CCM ambacho Serikali yake iliyomsimamisha awawakilishe na imeshamdharirisha hivyo pa sina ukweli?
Katika utetezi wake, Kibatala aliiomba mahakama imfutie mteja wake mashtaka kwa madai, hati ya mashtaka iliyowasilishwa mahakamani ilikuwa na upungufu mkubwa wa kisheria.
Alidai miongoni mwa upungufu uliokuwamo kwenye hati, ni pamoja na kutokuwa na maelezo yanayoonesha kosa alilokuwa akishtakiwa mteja wake.
Alidai vifungu namba 129 na 132 vya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai namba 20 kama ilivyorejewa na marejeo ya 2002, vinataka hati za mashtaka zizingatie na kutekeleza suala hilo.
Kwa mujibu wa Kibatala, kinyume cha hivyo, vifungu hivyo vinaipa mahakama uwezo wa kufuta hati ya mashtaka yenye upungufu wa kisheria.
Murji alisomewa mashtaka na Mwanasheria wa Serikali, Kisheni Mtalemwa akisaidiana na Zuberi Mkakatu, na kudaiwa Januari 19, 2013 katika maeneo ya Ligula Mtwara alichochea watu wafanye vurugu kinyume cha sheria.
Katika kesi hiyo, pia kulikuwa na washitakiwa 91 walioshitakiwa, na baadhi waliachiwa kwa dhamana na wengine walipelekwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti.
Murji pia alirudishwa rumande baada ya kukana mashitaka na kushindwa kutimiza masharti ya dhamana awasilishe mahakamani hati ya kusafiria, mdhamini mwenye mali isiyohamishika, yenye thamani isiyopungua Mil.20/- na ifanyiwa tathmini.
Pia alitakiwa asifanye mikutano ya hadhara bila kibali cha Polisi wa Mkoa, na kutokana na Murji kutokuwa na pasi yake ya kusafiria siku hiyo papo hapo ilishindikana.
Je alivyofanyiwa Murji na Serikali ya Chama chake, bado atakuwa na nguvu ya kuwatetea wananchi wake? Lakini wanajifunza nini katika hali kama hii? Tusiamshe hasira za wananchi bila sababu.
nyeregete@yahoo.co.uk 0715933308
No comments:
Post a Comment