BENKI ya NMB na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), wamezindua Huduma ya Uhakiki wa Dhamana za Zabuni za Kibenki Kidijitali ‘Digital Bank Guarantee VerificatiogÊ»n,’ itakayofanya kazi kupitia Mfumo wa Kitaifa wa Ununuzi wa Kielektroniki Tanzania (NeST).
Uzinduzi wa huduma hiyo inayoenda kurahisisha mchakato wa zabuni, uthibitishaji wa dhamana, kupunguza changamoto ya ufuatiliaji na kuimarisha Uwazi na Uwajibikaji, umefanyika jijini Dar es Salaam Alhamisi ya Machi 5, ukiingiza NMB katika rekodi nyingine ya kuwa Benki ya Kwanza nchini kutoa dhamana hizo kidijitali.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo, Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna, alisema kwa kutambua kuwa Ununuzi wa Umma ni moja ya nguzo kuu za shughuli za kiuchumi nchini, wameona waje na huduma hiyo ambayo wateja wataweza kuwasilisha na kuthibitisha dhamana za benki papo hapo.
“Kwa kushirikiana na PPRA, tunalenga kuhakikisha wateja na wadau wanapata huduma rahisi, ya kuaminika, na yenye uhakika zaidi, ambapo NMB tunaendelea kuthibitisha nafasi yetu kama mshirika mkuu wa kifedha katika kuendeleza mageuzi ya kidijitali na kuboresha utoaji wa huduma nchini.
“Ununuzi wa Umma ni moja ya nguzo kuu za shughuli za kiuchumi nchini, ambapo kila siku, makampuni makubwa, Biashara Ndogo na za Kati (SMEs), Wakandarasi, Wasambazaji na Watoa Huduma hushiriki katika Zabuni za Serikali zinazohitaji kasi, uaminifu na uzingatiaji wa taratibu na kanuni.
“Kwa muda mrefu mchakato wa dhamana za benki katika ununuzi wa umma (Bank Guarantee) ulikuwa na changamoto nyingi, ikiwemo matumizi makubwa ya karatasi bila kutumia teknolojia na mifumo ya mtandao, uhakiki kuchukua muda mrefu na kuwepo kwa hatari za udanganyifu au kupotea kwa nyaraka
“Uzinduzi wa huduma hii unalenga kutatua changamoto hizo na kuongeza uwazi na kurahisisha mchakato wa dhamana za benki kwa wateja wetu, ambao sasa wanaweza kuwasilisha na kuthibitisha dhamana za benki papo hapo, ikiwemo ‘Bid Bond,’ ‘Advance Guarantee’ na ‘Performance Guarantee.’
“Kwa lugha rahisi, mchakato uliokuwa unachukua siku kadhaa kukamilika, sasa utakamilika kwa muda mfupi sana na kwa mantiki hiyo makampuni makubwa na biashara ndogo na za kati katika sekta za ujenzi, usambazaji, na huduma, watanufaika vya kutosha kupitia huduma hii,” alisisitiza Zaipuna.
Aliyataja baadhi ya manufaa ya huduma hiyo kuwa ni pamoja na kushiriki zabuni kwa haraka na ufanisi zaidi, uthibitishaji wa dhamana papo hapo, kuondoa mzigo wa kiutawala, adha ya ufuatiliaji pamoja na kuimarika kwa uwazi na uwajibikaji, pamoja na kuongezeka kwa imani wakati wa kushindania zabuni.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba, aliishukuru NMB kwa kufungua njia miongoni mwa Taasisi za Fedha kuyaendea maono ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ya kutaka mifumo isomane ili kuwasaidia wazabuni ambao ni wateja wao kukamilisha michakato ya kuomba zabuni kwa urahisi zaidi na haraka.
“Tunamshukuru Rais Dk. Samia kwa maono yake mema kwa nchi yetu, ya kuhakikisha Sekta ya Ununuzi wa Umma inakuwa chachu ya Uchumi Jumuishi unaomgusa kila mtanzania. Kilichofanywa na NMB kupitia huduma hii ni kuungana nasi katika kuhakikisha maelekezo ya Rais yanatimia.
“Hatimaye leo tuko hapa kushuhudia uzinduzi rasmi wa uunganishaji wa Mfumo wa NeST na mifumo ya kibenki, na sasa tumeanza na NMB kutoa huduma ya kuwasilisha Dhamana za Zabuni za Benki kwa taasisi nunuzi kupitia Mfumo wa NeST.
Alisisitiza kuwa ujio wa huduma hiyo unaenda kuondoa kabisa mud awa taasisi nunu kuwasiliana na benki hiyo kwa nia ya kujiridhisha juu ya uhalali ama ubatili wa Dhamana ya Benki iliyounganishwa na mzabuni, hasa katika kipindi hiki ambacho michakato yote ya Tenda za Serikali inafanyika kupitia NeST.
“Mfumo huo kwa sasa unasomana na taasisi zaidi ya 20, sasa kutokana na mapinduzi haya, yataondoa kabisa muda wa taasisi nunuzi kuwasiliana na benki, badala yake mzabuni atatakiwa kuweka namba ya dhamana ya kibenki aliyopewa na Mfumo wa NeST utaivuta dhamana hiyo moja kwa moja kutoka benki.
“Haya ni mafanikio makubwa katika juhudi zetu za kuboresha mifumo ya ununuzi wa umma kwa kutumia teknolojia, na kuimarisha uwazi, ufanisi, na usalama wa dhamana za kifedha zinazotumika katika michakato ya zabuni na usimamizi wa mikataba,” alisema Simba.
Aliongeza kuwa, Ununuzi wa Umma ni nyenzo muhimu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya taifa, na kwamba ili kulinda rasilimali za umma, taasisi nunuzi zinahitaji dhamana za kifedha kutoka kwa wazabuni na wakandarasi, ikiwemo dhamana za zabuni, dhamana za utekelezaji wa mikataba, na dhamana za malipo ya awali.
“Dhamana hizo hutoa uhakika kwamba mzabuni au mkandarasi atatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa makubaliano. Hivyo natangaza rasmi kwamba kuanzia mwezi huu wa tatu (yaani Machi 2026), Huduma ya Uhakiki wa Dhamana za Zabuni za Kibenki za NMB Kupitia NeST itaanza kutumika kwa wazabuni wote,” alisema.




No comments:
Post a Comment