Na Salum Mkandemba
MRATIBU Taifa wa Mtandao wa Mashirika ya Haki za Binadamu
Kusini mwa Afrika (SAHRINGON Tanzania), Martina Kabisama, amezitaka Asasi za
Kiraia nchini kusaidia Watanzania katika mchakato wa Katiba unaoendelea ili
kuepuka matakwa ya wanasiasa kugubika mchakato huo.
Martina alitoa wito huo jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa
akichangia mada katika Mkutano wa Asasi za Kiraia za Afrika Mashariki (EACSO),
ulioratibiwa na Chama cha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Tanzania (TANGO),
kujadili mambo kadhaa, ikiwamo Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Aliongeza kuwa, katika Mkutano Mkuu wa Global Social World
wa mwaka 2011, pamoja na mambo mengi, Afrika ilishauriwa kuwa na Asasi za
Kiraia zinazoshiriki kwa mapana kuwasaidia wananchi katika michakato ya katiba
na sio kukurupukia matakwa ya watawala wa nchi.
“Asasi za Kiraia Tanzania zinapaswa kujifunza kutoka kwa
asasi kama hizo za Kenya katika kuwezesha upatikanaji wa katiba inayomtambua na
kumthamini Mtanzania masikini, sio kuegemea katika malumbano ya kujadili hatima
ya Muungano na kusahau mambo muhimu,” alisema Martina.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Dira Afrika
Mashariki (Vision East Africa Forum), Dk Azaveli Lwaitama, alizitaka Asasi za
Kiraia nchini kutohofia tofauti ya kiuchumi baina ya nchini za Jumuiya ya Afrika
Mashariki, kwani zina nafasi sawa katika kunyanyua maendeleo ya nchi hizo.
Dk Lwaitama alibainisha kuwa, moja ya changamoto
inayoikabili Jumuiya ya Afrika Mashariki ni tofauti ya kiuchumi baina ya
mataifa na watu wake, ambayo imo hata miongoni mwa wananchi wa nchi moja, hivyo
Asasi za Kiraia zinapaswa kuwaongoza Watanzania kujifunza kutoka kwa wenzao.
“Tofauti ya kiuchumi ipo, lakini Watanzania hatupaswi
kuihofia, badala yake Asasi za Kiraia zisimame katika kufanikisha kuwapo kwa
mchakato wa Katiba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ili kuwawezesha Wanajumuiya
kunufaika ipasavyo,” alisisitiza Dk Lwaitama.
Aliongeza kuwa, Katiba ya Jumuiya hiyo, itasaidia uharaka wa
maendeleo kwa nchi wanachama, kupitia uwekezaji wa pamoja utakaofanikisha kurejea
kwa Mamlaka za Usafiri Majini, Sarafu ya Pamoja na Mashirika ya Reli na Ndege
ya Afrika Mashariki.
No comments:
Post a Comment