Na Bryceson Mathias, Lukunguni Kikeo, Mvomero
MLOKOLE Delvanus Jeremia (29) aliyechaguliwa kuwa Katibu wa Kamati ya kuandika Majina ya waliogawiwa Vocha za Mbolea Lukunguni Kata ya Kikeo, amejiuzulu.
Jeremia alijiuzulu Ukatibu wa Kamati hiyo hivi karibuni, akidai hayupo tayari kufanya kazi ya kuwaorodhesha wakulima waliopokea mbolea, kutokana na kuwepo tuhuma za Ufisadi.
Alipohojiwa na Mwandishi, Jeremia alithibitisha kuandika barua kwa Mtendaji wa Kijiji hicho, ikiwa ni siku moja baada ya Wakazi wa Lukunguni na Vijiji Jirani kuulalamikia Uongozi wa Kata Kikeo na ule wa Kilimo Mvomero, kuwa umechakachua Mifuko 600 ya mbole ya 2012/2013 na kutishia kutimkia Chadema.
Akifafanua kujiuzulu kwake Jeremia alisema ni kuwepo kwa Maelezo yanayolalamikiwa kwamba baadhi ya viongozi wa Kilimo Mvomero na Kata ya Kikeo, wanashinikiza kuwa wakulima walipata mifuko 450 ya Mbolea ya 2012 na 2013 wakati wananchi wanakataa.
“Sitaki kuhusishwa na Jambo lolote la Vocha za Mbolea kwa sababu kuna malalamiko na manung’uniko ya wakazi wa Lukunguni na vijiji jirani kikiwemo cha Lware tulipofanyia mkutano na viongozi wa Kilimo Wilaya ya Mvomero wakidai hawajapata mbolea hiyo".alisema.
Aliongeza kuwa, Sababu ya pili ya kujiuzulu ni kuwepo minong’ono na tuhuma ya majina ya waliokufa ambao wamedaiwa kuorodheshwa kuwa wamepata mbolea, jambo ambalo kwa kuwa yeye ni mgeni na ana miezi sita tu, hawezi kuwatambua watu wote.
Alidai, kutokana na sintofahamu hiyo, amemwandikia Mtendaji kujiuzulu Ukatibu huo ya 13.03.2013 ili kujiepusha na tuhuma hizo, hasa akizingatia Uadilifu wake kama Mlokole wa Kanisa la Assemblies of God kuwa linakinzana na kile kinacholalamikiwa.
Aidha alisema, Kijiji cha Lukunguni kina wananchi 3,000 na wanaofanya kazi za maendeleo kwa Taifa ni 1,800; hivyo haoni vema kukubali pendekezo lililofanywa na Viongozi wa Kata na wale wa Wilaya ya Mvomero, ambapo alidai, kama akiorodhesha majina ya uongo kwa matakwa ya wachache na si ya wengi, atakuwa amemkosea Mungu.
No comments:
Post a Comment