HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 12, 2013

ZIARA YA KINANA CHINA, AFANYA MAZUNGUMZO NA VIONGOZI WA CPC

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana (wa pili kulia) akimtambulisha Katibu wa CCM mkoa wa Mbeya Maganga Sengelema, kwa Katibu wa kitengo cha kusimamia maadili wa Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC), Huang Xianyao, Kinana na ujumbe wake walipokuwa na hafla maalum iliyofanyika Machi 11, 2013, katika hoteli ya Dongfang Jimbo la Guangzhou, China. (Picha na Bashir Nkoromo)
 Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akimkabidhi zawadi ya kinyango cha Kimakonde,  Katibu wa kitengo cha kusimamia maadili wa Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC), Huang Xianyao,  Kinana na ujumbe wake walipokuwa na hafla maalum iliyofanyika Machi 11, 2013, katika hoteli ya Dongfang Jimbo la Guangzhou, China.

NA BASHIR NKOROMO, CHINA


KATIBU Mkuu wa Chama CHa Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana amekiomba Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC) kuhimiza wananchi wa China kuchangamkia fursa ya kuwezeka nchini Tanzania.

Alisema, Wachina kuwekeza na kushiriki shughuli nyingi za kiuchumi Tanzania ni miongoni mwa kiunganishi kikubwa kitakachoweza kudumisha urafiki na undugu wa siku nyingi kati ya nchi hizo mbili ambao hadi sasa ni wa kupigiwa mfano duniani.


Kinana alisema hayo , Machi 11, 2013 wakati akizungumza na Katibu wa Kamisheni ya Maadili ya Chama Cha Kikomunisti cha China, Huang Xianyao, katika hafla maalum iliyokutanisha Kinana na ujumbe wake na baadhi ya viongozi wa CPC, kwenye hoteli ya Dongfang, jimbo la Gwanzhou nchini China.


"Hivi sasa Tanzania imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji, hivyo ninyi ndugu zetu wa China, ni vema mkaitumia fursa hii kuwekeza. Hii itazidi upanua zaidi wigo wa mahusiano ya kirafiki tulionayo kwa miaka mingi sasa", alisema Kinana.

Kinana alisema, baadhi ya maeneo ya uwekezaji yanayoweza kuleta tija katika uchumi wa Tanzania na China ni Kilimo, kwa sababu hivi sasa Tanzania imejizatiti sana katika sekta hiyo ili kuifanya kuwa nyenzo ya uhakika kuinua na kukuza uchumi.


Akizungumza na Kinana, Xianyao alisema, China inatambua fursa za kiuchumi zilizopo Tanzania, na ipo tayari kuzitumia fursa hizo, kwa kuwa mbali na kuleta faida kwa Tanzania lakini itasaidia pia kuinua uchumi wa China na watu wake.


Alisema, licha ya China kuwa na changamoto za kijamii ikiwemo ukosefu wa ajira kwa vijana wake, lakini imejitahidi kupambana na changamoto hizo chini ya uongozi imara wa CPC na sasa ni moja ya nchi zilizopiga hatua kiuchumi duniani.


Xianyao alisema, China imeweza kupiga hatua kutokana na kujikita katika uchumi wa soko, kilimo cha kitaalam na viwanda na sasa imeweza  kufanya idadi kubwa ya wananchi wa China kusihi maisha ya nafuu mbali ya changamoto ambazo ni lazima kuwepo.


Katika ziara hiyo Kinana amefuatana na Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar), Vuai Ali Vuai, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Khadija Aboud, Katibu wa NEC, Siasa na Uhuaisno wa Kimataifa, Dk. Asha-Rose Migiro, Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM, Martine Shigela, Katibu Mkuu wa Jumuia ya Wazazi, Khamis Suleiman Dadi, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mjini Magharibi na Mohammed Yusuf Mohamed.


Wengine ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa,  Jesca Msambatavangu, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu Titus Kamani, Katibu wa CCM mkoa wa Mbeya Maganga Sengelema na maofisa wa Chama.


Kinana anafanya ziara ya siku kumi nchini China kutokana na mwaliko wa Chama Cha Kikomunisti cha China, na anafanya ziara hiyo ikiwa ni ya kwanza kuifanya nje ya nchi, tangu alipoteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Oktoba mwaka jana mjini Dodoma.

CPC imemwalika Kinana ili kupata fursa ya kubadilishana uzoefu kisiasa na katika nyanja za uchumi ambapo kwa upande wa CCM itapata fursa kubwa ya kushuhudia jinsi gani China imeweza kupiga hatua katika uchumi wa nchi hiyo.

No comments:

Post a Comment

Pages