Askari wa jeshi la polisi mkoani Mtwara wapo katika hali
mbaya ya kuishi baada ya kutimuliwa toka uraiani na kulazimishwa kuishi kambini, baada ya
kutofautiana na wananchi katika sakata la gesi lililofanya Askari kuelekezwa
kukamata na kupiga baadhi ya wananchi.
Chanzo chetu cha habari kimethibitisha kuwa tarehe 17 June
wiki iliyopita kamati ya Ulinzi na
Usalama ya mkoa ilifanya kikao ikiwa na baadhi ya viongozi wa jeshi la
wananchi, na viongozi mbalimbali wa serikali, walimwomba Kamanda wa polisi wa
mkoa Linus Sinzumwa kuomba radhi kwa niaba ya Askari wake waliofanya vitendo
vya kihalifu dhidi ya raia.
Katika sakata hilo wananchi hawakukubali, badala yake
waliwaomba Askari wote wahame uraiani wakaishi kwenye kambi zao na nyumba zao
ambazo kimsingi hazitoshi kuwezesha malazi kwa Askari wote.
Taarifa zaidi zinasema Askari walioko Mtwara wamelazimika
kuishi katika mahema waliyogawiwa na kuyaweka katika maeneo ya Line polisi,
mahali ambapo wanadhani ndio salama kwao.
Uhusiano kati ya jeshi la polisi na raia unadaiwa kutetereka
hadi kutouziwa baadhi ya bidhaa muhimu kwa ajili ya chakula, na raia yeyote
anayebainika kutumwa kununua kwa ajili ya askari anaadhibiwa na raia wenzake.
No comments:
Post a Comment