Na Elizabeth John
LICHA ya serikali kuingiwa na hofu ya kupeleka timu Sudan kushiriki michuano ya Kagame, Kocha Mkuu wa klabu ya Simba, Abdallah Kibadeni amesema anaiunga mkono na ni vema kuangalia hali ya usalama kwanza.
Mashindano hayo yanayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) yamepangwa kufanyika nchini humo kutokana na serikali yake kuhakikisha hali ya usalama kutokana na kuwa na mapigano kwa muda mrefu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kibadeni alisema timu yake inaendelea na mazoezi kama kawaida hata kama serikali itazuia timu hizo kushiriki wataendelea kujiweka sawa na michuano mingine.
“Usalama ni kitu cha kwanza alafu mambo mengine yanafuata, itakua haina maana vijana wetu waende huko afu hali ibadilike,” alisema Kibadeni.
Alisema timu inaanza mazoezi rasmi leo na amewataka wachezaji ambao wapo mbali warudi haraka ili aweze kupanga kikosi ambacho kinaelewa.
Tanzania inawakilishwa na Yanga ambao ndio bingwa mtetezi wa michuano hiyo na Simba kama bingwa wa bara msimu uliopita.
Simba iko kundi A na timu za El-Merrikh (Sudan), APR (Rwanda) na Elman (Somalia) wakati Yanga iko kundi C sambamba na Express (Uganda), Ports (Djibout) na Viatal’O (Burundi).
Michuano hiyo imekuwa ikifanyika chini ya udhamini wa Rais wa Rwanda, Paul Kagame, ambaye huto zawadi kwa mshindi wa kwanza hadi wa tatu.
No comments:
Post a Comment