HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 23, 2013

Kwa nini Mbowe alazimishwe kuwasilisha ushahidi bomu la Arusha?

Ukitaka asali, Jiandae kukabiliana na Nyuki!

Na Bryceson Mathias
 
HIVI karibuni Jeshi la Polisi lilimtaka Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kuwasilisha ushahidi unaoituhumu Polisi kuhusika na mlipuko wa bomu lililolipuka katika mkutano wa chama hicho viwanja vya soweto, jijini Arusha Juni 15, mwaka huu.

Wakati Polisi ikiendeleza Shuruti hiyo, tayari CHADEMA kilishakataa kutoa ushahidi huo kwa polisi kikidai kinamtaka Rais Jakaya Kikwete aunde tume huru ya Kijaji itakayosikiliza shauri hilo.

Ijapokuwa Mbowe na Chama chake kililituhumu Jeshi hilo kuhusika na mlipuko, na kikaahidi kutoa ushahidi unaong’ang’aniwa na Polisi kwa kwa Sharti la Rais Kikwete kuunda tume huru ya kijaji, kwa nini walazimishwe kwa mikiki wakati Polisi walikuwako kwenye tukio?

Inakuwaje Polisi waliokuwepo kwenye Mkutano wasione Ushahidi wanaoudai, halafu Raia na Mbowe waone, halafu utake msaada kwao kwa kutoona kwako ukiwa kazini kwa vitisho na shuruti? Tuseme basi Mbowe na Raia wana Ustadi wa Kipolisi kuliko Makachero?

Ukiwa na Janga la njaa nyumbani kwako na kufika kwa jirani yako mwenye chakula, huwezi kumlazimisha kwa nguvu ya matakwa yako au shuruti akupe chakula chake kirahisirahisi, wakati mvua iliponyesha ulikuwepo, lakini ukapuuza kulima!

Ingawa ipo Sheria na Utu wa kutomnyima chakula mtu mwenye njaa ili asife, lakini mwenye njaa hawezi kumlazimisha mwenye nacho kwa kutumia maguvu ili aogope na kumpa chakula, ambacho yeye hukukisotea kukitafuta!

Kukitafuta chakula kuna gharama yake, tangu kutayarisha shamba, kulima, mbegu, kupanda, kupalia, kutunza, kama ni Mpunga ili upate ubwabwa kuna kuamia ndege, madawa, kuvuna na hatimaye kula.

Hivyo ili kupata chakula kisichochako, kinahitaji unyenyekavu wa kujieleza na Utu wa kumuomba mwenye nacho, ili hatimae aelewe na apate huruma ya kuamua kukupatia bila shuruti na kinyongo.

Matunda mengi mazuri, huwepo kwenye miti yenye miiba mikali na kama haina miiba basi, ipo ya kukwea; na kama ni ile ya kupandwa na kustawishwa na mtu shambani kwake au nyumbani, basi inahitaji unyenyekevu kama nilivyotangulia kusema.

Kwa msingi huo ukitaka kuchuma au kuangua matunda ya namna hiyo, kuna kazi au gharama ambazo ni lazima uziingie! Moja ni kuupenyeza mkono kwa uangalifu ili ulifikie tunda na kulichuma bila kuchomwa na miiba, kulishikilia vizuri ili lisidondokee pachafu, likaharibika au kukosa radha.

Waswahili wanasema, Ukitaka asali, Jiandae kukabiliana na Nyuki, ili ubora na utamu wa asali ubaki palepale bila kuharibika au kupoteza radha yake, na hatimae ipelekee kuwepo kwa uwezekano endelevu wa kupata asali kila mara.

Ingawa ili kuvuna asali ki-analojia unaweza kuvuna asali kwa moto ukitumia moshi kuwafukuza nyuki, jambo ambalo kimsingi unaweza kuharibu asali na kupoteza radha yake ikiwa ni pamoja na kuua virutubisho.

Utalaam mwanana wa kulina asali kidijitali, huhitaji kutumia moshi, lakini kosa la Jeshi la Polisi na Watawala, wamekuwa wakitumia Nguvu ya Mabomu ya Machozi kupata Amani (Asali), jambo ambalo limesababisha Mauaji na Ulemavu na Amani kutoweka, huku wananchi wakiichukia Serikali yao.

Hali hiyo ya Mikiriti ya Polisi, Vikundi vya Ukakamavu vya Kiutawala na Nguvu za wana siasa wa Chama Tawala na Kiti cha Spika, ndivyo vimesababisha kukosekana kwa Demokrasia ya kweli nchini, hali inayolalamikiwa na Wanahabari, vyombo vya haki nchini na nchi za Nje.

Sielewi kwa nini Watawala, Vyombo vya vya Dola vinajifanya havielewi Uzalendo na Mustakabali wa Utu wa Mtu. Kama hata shahidi mahakani ili akasaidie kutoa Ushahidi anaombwa kwa hekima na unyenyekevu ili kushinda kesi! Inakuwaje Dola na Watawala kwa Mbowe na Chadema washindwe?

Shahidi kila siku hugharimiwa Usafiri, Chakula, Malazi na chochote kinachomfanikisha Shahidi atoe maelezo yenye kumfanya Mshitaki au Mshitakiwa aweze kushinda kesi! Je inakuwaje kwa Mbowe na Chama chake?

Je Hatuwezi kuwatendea utu wa namna kama hiyo tufanikiwe kumpate mbaya wetu wa Mabomu aliyeua ndugu zetu katika mkutano wa chama hicho viwanja vya soweto, jijini Arusha?

Aidha barua za vitisho kama kumbukumbu ya jalada, AR/IR/6223/2013 ya 17, Julai 2013 ya Kamishna Msaidizi wa Polisi, Hussein Laisseri, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai inayomtaka Mbowe apeleke vielelezo kwa mujibu wa kifungu namba 10 (2) na (2A) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai, havisaidii kutatua tatizo.

Hapa panatakiwa kuwa na ushirikiano wa kidugu, na utendaji wa kazi kwa masaidiano bila kuviziana kwa kukamatana na kurushiana maneno machafu yenye kuudhi kama ya Paulo chagonja kwa Mbowe na Chama chake.

Ieleweke, Watanzania wanataka kumjua mbaya aliyehusika kuwaua ndugu na wananchi wenzio, hawataki Itikadi, Cheo cha Mtu, Nafasi yake au Nguu za Dola. Vinapopnyezwa vitu hivyo, ndipo tunapopata tabu kuwafahamu! Wanaingia mafichoni.

Ninachofurahi, ‘Mbowe hajasema hatoi ushahidi, atatoa; lakini si kwa polisi, anataka tume huru ya kimahakama ya kijaji, ambayo inapaswa kuundwa na rais, sasa rais hajasema hataunda, Jeshi la Polisi linapolazimisha watanzania tunashindwa kuielewa polisi’

Kama Chadema wameeleza polisi kuwa hawatawasilisha ushahidi wao kwao kwa kuwa wanaamini wao ni watuhumiwa namba moja, wana hofu gani? Na kimsingi polisi hawakupaswa kumshika Mbowe bali kamati kuu iliyoamua kutoutoa ushahidi huo kwa polisi.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa nyeregete@yahoo.co.uk

0715933308

No comments:

Post a Comment

Pages