HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 07, 2013

Kwa nini Watawala wakiombwa Yai wanatoa Nge?

Na Bryceson Mathias
UBWATUKAJI na vitisho vya maneno yanayowachochea wananchi kuichukia serikali yetu sikivu, sasa ifike mahali ifikirishe na kuamsha ubongo na ufahamu, kwa nini kama Watawala,  wakiombwa Yai hutoe Nge?
Biblia Luka 11:11-12 ”Kila aombaye hupokea; atafutaye huona; abishaye atafunguliwa. Ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe , badala ya samaki atampa nyoka?  Au akimwomba yai, atampa nge?”
Watawala wakifika mahali wanasema wamechoka, maana yake hawawezi na wanapaswa wasaidiwe, kwamba hawataki kujibu hoja na tuhuma zinazoelekezewa na wanasiasa wenzao kuhusu Uzembe, Kukosa Weledi na Kutowajibika.
MUNGU aliwaamuru wana wa Israel, Wasiabudu Miungu Mingine ambayo hata hawajawahi kuijua ambapo alisema,
“Angalieni, leo hii nawawekea mbele yenu baraka na laana, Baraka kama mtatii amri za Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, na laana, kama hamtazitii amri za Mwenyezi – Mungu, Mungu wenu,  ambazo nawapeni hivi leo”
Wakati Wamachinga na Walalahoi wa Mwanza wakipumbazwa na Usemi kama wa Mama Yakobo na Esau, alipodanganya kwa hila kumfanya Yakobo awe na Manyoya ya Esau, ili Baba aliyekaribia kufa ambarika Yakobo badala ya Esau!
Nyerere alisema,"Lakini ni vizuri nikasema pia kwamba kwa maoni yangu, hatuwezi tukaamua kuacha mfumo wa Demokrasia ya Chama Kimoja, tukajaribu mfumo wa Demokrasia ya Vyama Vingi kwa matumaini ya kwamba;
“Tukikuta kuwa mfumo huo hautufai, basi tutarudia tena Demokrasia ya Chama Kimoja. Tutajidanganya, haiwezekani na ni vigumu kabisa! Ukimwacha mkeo ukaoa mwingine, na ukagundua kuwa huyu wa pili ni balaa, ni vigumu kumrudia mkeo wa kwanza.
“Demokrasia ya Vyama Vyingi ikitushinda, mfumo ambao ni rahisi kufuatia utakuwa ni udikteta wa mtu mmoja au utawala wa kijeshi. Hiyo ni sababu nyingine muhimu ya kutofanya uamuzi kwa pupa”.
Leo miaka 21 ya Demokrasia ya Vyama Vingi ambayo Chama Tawala ilijigamba, asilimia 80% ya Watanzania ilikataa mfumo huo, na 20% kubali, hivyo iliona wachache wakubaliwe, na mfumo ukaanzishwa.
Leo Inatisha 20% inapokua kukidhi ridhaa iliyolazimishwa, walioridhia, hawataki mtoto vyama vingi akue, na ikibidi afanane na waliomtangulia kiafya, hivyo akiomba Samaki anapewa Nyoka mwenye sumu afe!
Kama mtoto anaomba Mkate anapewa Jiwe, ina maana hatakiwi akue ila ilidhaniwa adumae na kubaki asilimia 20% ya utoto, akitumwa sokoni, kufagia Uwanja na kuchunga Ng’ombe asije akaoa akawa Baba au Mama mwenye Nyumba
Nyoka na Nge ninayemkusudia, ni Mabomu ya Machozi, hila za kuzuia Mikutano ya Siasa, kudai haki, Nguvu za Dola kupita kiasi cha kuua watu, kujeruhi na kusababishia ulemavu; Hali hii ni sawa na kuoza mtoto ukazuia aliko asizae!
Ukiachia Mikoa ya Mwanza, Kilimanjaro, Iringa, Mbeya, Arusha, Mara, Kagera, Dar es salaam inayofahamu andika la Biblia Mhubiri 5:10-11
 “Apendaye fedha hatashiba fedha, Wala apendaye wingi hatashiba maongeo. Hayo pia ni ubatili.Mali yakiongezeka, hao walao nao waongezeka na mwenyewe hufaidiwa nini, ila kuyatazama kwa macho yake tu?”. Iliyosalia bado hupumbazwa na Kanga, Iishti na Ubwabwa Harambee, kama kwa Chama Kimoja.
Washindani wanapostawi, tukaanza kuwaua kwa hila za Harambee na kuzuia mikutano yao, basi kama alivyosema Nyerere, Tutajidanganya, tulifanya uamuzi kwa pupa, hivyo hatuna Dira ya Maendeleo, tumebaki Chumvi ya kutupwa nje na kukanyagwa na watu.
nyeregete@yahoo.co.uk 0715-933309

No comments:

Post a Comment

Pages