HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 30, 2013

Kwa nini watu watozwe kiingilio UBT, wakati huduma hakauna?

Na Bryceson Mathias

WANANCHI, wanaosafiri na wanaosindikiza  ndugu zao katika Kituo cha mabasi yaendeo mikoani na nchi jirani (UBT), wanaendelea kutozwa kiingilio kile kile katika kituo pamoja na kutopata huduma zinazostahili.

Kama utasafiri na kufika UBT kama nilivyofanya mimi, utashuhudia uchafu wa uchafu  wa maji machafu yanayonuka, utiririkaji  ndani ya Kituo  hicho, ambapo yanatuama na hadi kubadilika rangi na kuwa ya kijani ambayo ni hatarishi kwa afya za wote kituoni humo.

Lakini pia, hali ya usalama ndani ya kituo hicho inatia shaka maana kwa tusema kwa ujumla usalama ndani ya kituo ni tete, na jambo ambalo linatishia Mali na Maisha ya abiria na dhidi ya matukio ya uhalifu ambayo yamesababisha madhara kwa abiria na wasindikizaji pia.

Ni hoja yangu kwa Mkurugenzi wa Jiji Dar es Salaam Dr. Didas Masaburi, kama maji hayo machafu yangekuwa yanatiririshwa nyumbani kwake, angechukua hatua gani? Majibu anayo.
Najua angechukua hatua za haraka.

Kama hivyo ndivyo, basi hatua hizo hizo zichuliwe sasa kwenye Kituo cha Mabasi ya Ubungo Bus Terminal (UBT), ambapo watu hohehahe na wasio na sauti ya kupiga kelele, wanaumia kwa adha hiyo.

Je, uchafu wa namna hiyo ungekuwa unatiririka karibu na nyumbani ya Meya wa Jiji la Dar es Salaam, si hatua zingechukuliwa haraka na pengine bila hata vikao wala ushirikishwaji. Roho hii isipothibitiwa tutauana kwa kutegemea dharura hadi tuishe.

Labda pia niwahoji watendaji wa Halmashauri ya Jiji Dar es Salaam. Hivi kama maji machafu ambayo yananuka na kubadilika kuwa kama Kijani, yangekuwa yanatiririka ofisi mwao, wangechukua hatua gani?

Nina uhakika vikao maalumu au dharura vya Kamati ya Fedha na Uongozi na pengine  Baraza la Madiwani, lingekaa haraka kuwezesha kufanyika maamuzi na hatua za haraka kuchukuliwa kuondokana na harufu hiyo. Lakini kwa sababu UBT ni kwa walalahoi, hakuna maana!

Hivi kwa mfano, kipindupindu au magonjw ya mlipuko yakiibuka na kuua watu wengi Ubungo, alaumiwe nana? Najua kwa kawaida ya viongozi wetu walivyo. Wanataka hadi watu Lundo wafe ndipo waanze kuhaha kuchukua hatua!

Nashangaa viongozi wetu, kila siku hapa nchini, sasa tumekuwa tukiimba tutoke analojia tuingie digitali, huku ndiko kuhama na kuingia undawazi mpya? Mpaka kusababishwe maafa, majanga,kuibuke mgogoro au maandamano baina ya Serikali na Wananchi,, watu wapigwe mabomu, ndipo ifanyike.
Kimsingi tunajua kwa nini watawala wanatamani kuchukua hatua za utekelezaji hadi kutokee maafa, majanga au vurugu. Ni kwa sababu humo ndimo watu wanafanya ufisadi unaotokana na dharura wakiwapumbaza wananchi kote nchini.

Jambo lingine ambalo haliwezi kuachwa bila kusema kuhusu kituo cha Mabasi (UBT), ni  kutozwa kwa kiingilio UBT kwa safari na wasindikizaji, wakati huduma za msingi kwa mazingira ya binadamu hakuna.

Mbali ya ukosefu wa huduma, lakini kiwango cha kiingilio hicho, ni kilekile kilichokuwa kikitozwa wakati ndani ya UBT kulikuwa na huduma zote za msingi kwa binadamu. Nilitegemea kwa kuwa huduma za msingi hakuna, basi gharama yake ingepungua au kuondolewa kabisa.

Inapofika serikali inaruhusu hayo kufanyika, basi ndani mwake kuna rushwa na ufisadi mkubwa wa kubebana, ambao kimsingi hauna dawa zaidi wananchi kuona wadhulumiwa haki yao mchana kweupeeee!

Hayo yakiachiwa yafanyika namna hiyo, yanazidi yanazidi uchafu UBT.

No comments:

Post a Comment

Pages