Kukiwa kumebaki siku mbili kabla ya kufanyika uchaguzi wa Madiwani mkoani Arusha, kuna tetesi wananchi na hasa wenye Shahada, wamekuwa wakitakiwa na Mabalozi kuorodhesha Namba za shahada za kupigia kura kwa Mabalozi wao.
Tetesi na Malalamiko hayo zimetolewa na baadhi ya wakazi wa Kata ya Kaloleni, wakidai kutishiwa kuhamishwa Kata na Mabalozi wa Nyumba 10 wanaopita majumbani usiku kufuatia kugoma kutoa shahada zao ziorodheshwe namba.
Mbele ya wandishi wa habari Kaloleni Arusha, Imedaiwa Balozi wa Nyumba 10 Kata ya Kaloni Magharibi, Edington Mshana alisema walipewa maagizo na Katibu wa Tawi la CCM Kaloleni Magharibi, Kata ya Kaloleni, Erinesta John.
Najiuliza, Katibu Kata huyo (John) ni nani katika nchi hii hadi ataka Shahada za watu? John ametumwa na nani kukusanya namba za Zahada hizo? Kwa nini namba za shahda hizo ataka kukusanya usiku na si mchana? Je huyo ni Mwanga au Jini afanye kazi hiyo usiku?
Nyakati hizo Jogoo alikuwa na Macho na Nyoka alikuwa na Miguu. Kila siku sherehe ilipotokea katika eneo lao, Jongoo alimpitia Nyoka na kumchukua akimuongoza hadi kwenye sherehe, huko alikia tu uzuri wa Sherehe, yanayofanyika hakuona!
Siku moja Nyoka alipanga mbinu, akajiuliza, nitawezaje kumnyang’anya macho Jongoo ili niweza kuona raha za Sherehe naye achukua miguu yake? Nyoka akapata jibu. Udanganyifu huo ataufanya wakiwa nyumbani si kwenye sherehe, maana atamshitukia!
Siku ya pili Nyoka alidamka mapema usiku usiku, akabisha hodi kwa Jongoo, akamuuliza leo unakwenda wapi? Jongoo akasema, siendi kokote nitakuwa hapa hapa, nina kazi kidogo ya kufanya!
Nyoka! Niazime macho yako niende kwa mdogo wangu maana wanakwenda kulina asali ili nyuki wasije wakaniuma! Nikirudi, nitakurudishia macho yako, tena sitasahau kukuletea Masega ya Asali, nawe uburudike.
Jongoo kusikia ataletewa Asali, alikubali Uongo huo akampa Nyoka macho, naye achukua Miguu Mingi ya Nyoka akaijaribu, kama unavyoweza kutoa Shahada ukapewa Kofia, Kanga , Skafu au Ubwabwa!
Jongoo alikuwa anatambaa kwa tumbo huku miiba na Nyasi zikiumsumbua, alishangaa siku ile hata mchanga ambao huwa unakuwa wa Moto kwa jua kali na kumuunguza, siku hiyo haukumathilri, akabaini labda ukiwa na miguu tumbo linakuwa juu, haungui tena.
Nyoka naye alisikia furaha, kwa sababu kwa mara ya kwanza aliweza kuona nuru na usiku ule alifanikiwa kuuona mwezi ukizama asubuhi, na alipotoka na kwenda shimoni, wenzake walimshangaa kwa kuwa ana macho.
Toka hapo Nyoka hathubutu kukaribiana na Jongoo, asije akamnyang’anya macho, ndiyo maana hadi leo, Nyoka hawapatani na Jongoo, na Jongoo akiguswa hata na unyasi kichwani, hujikunja akidhani amerudishiwa macho na nyoka ili ayafiche, Nyoka asiyachukue tena!
Wananchi na Wapiga Kura wa Kata za Arusha, Msidanganyike na Uongo wa Nyoka kuwa anaazima Shahada zenu ili zikamsadie kuona Shehere kwa Mdogo wake! Mtalia! Mtakosa Maendeleo, Mtakosa haki zenu na Ustawi mzima wa Maisha yenu!
Shahada ni Hospitali(Afya), Shahada ni Shule (Elimu), Shahada ni Uchumi (Kipato), Shahada ni Daraja (Kuvuka), Shahada ni Maji ya Kunywa( Uhai), Shahada ni Chakula, Shahada ni Nyumba (Kulala), Shahada ni Ardhi (Kulima), Shahada ni Utajiri na ni Gari!
Mtu awaye yote anayekudanganya umpa Shahada, anataka uhai wako, anataka watoto wako, anataka kuharibu maisha yako, anataka ufe, anataka uugue, anataka usilime, anataka uwe maskini na kadharika na kadharika.
Hiyo sherehe ya John na Uongo wake Nyoka yaani, Kanga, Kofia, T-sheti, Skafu, Ubwabwa na Nyama ya Kuku ya siku Moja, na tufedha kidogo twa kutumia siku moja, ni umarehemu wa Miaka mitano, labda upate Muujiza wa kufufuliwa kama Lazaro kwa Yesu.
Watu kama John wanaoomba Shahada yako, ni Waongo maana wanaomba macho yako ili uwe Kipofu wao wanaona, uambulie Giza. Ukithubutu kumpa Johna Shahada, umempa Macho, hata kama utadhani ukipokea miguu yake utakuwa juu ya Mchanga unaochoma, Umekufa inagawa uko hai!
Ukidanganyika kutoa Shahada, utabaki kuwa kama Jongoo, ukijigusa kwenye Nyansi utadhani Nyoka anakurudishia Shahada hivyo utajikunja kama unaficha ili asiichukue tena, lakini bure utakuwa Mtumwa wa Nyoka. Aheri Jongoo alimfuata na kumtembeza Nyoka, wewe Utabaki Hoi!
Chonde Chonde Mwananchi na Mpiga Kura Ujue hayo, na raia yangu watu wa Arusha Msidanganyike
|
No comments:
Post a Comment