Na Ferdinand Shayo,Arusha
Wakulima wameshauriwa kujenga tabia ya kuvuna maji ya mvua na kuyatumia katika shughuli za umwagiliaji hasa katika kipindi ambacho mvua ni chache na haziendani na kalenda ya wakulima.
Kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo yamekuwa yakipelekea kukosekana kwa mvua za kutosha na uharibifu wa mazingira nao umetajwa kuwa sababu ya tatizo hilo.
Hali hiyo imekuwa ikipelekea wakulima kupata mazao kidogo ama kutovuna kabisa jambo ambalo limekuwa likisababisha baadhi ya maeneo nchini kuwa hatarini kukubwa na baa la njaa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika mafunzo yanayolenga matumizi ya muongozo kabambe wa umwagiliaji kwa wataaalamu wa kilimo katika mikoa ya kanda ya kaskazini na kati yaliyofanyika jijini hapa, Afisa Kilimo Mkuu Bwana Amana Mbowe kutoka Ofisi ya umwagiliaji kanda ya Kilimanjaro amesema kuwa ni vyema wakulima wakajenga tabia ya kuvuna maji ya mvua na kuyatumia hasa kwa njia ya kujenga mabwawa na kuyahifadhi.
Vile vile amependekeza njia nyingine ya kutumia maji ya ardhini kwa kuchimba visima virefu na vifupi ambavyo vitawasaidia kulima na kupata mazao mengi badala ya kutegemea mvua ambazo ni chache na haziji kwa wakati zinapohitajika.
Bwana Mbowe amesema kuwa serikali kwa kutambua umuhimu wa kilimo cha umwagiliaji tayari imeanzisha mpango wa muongozo kabambe wa umwagiliaji kitaifa ambao uko katika utekelezaji ,na wameweza kuanzisha mabwawa sehemu za Muhenza na skimu ya Mombo.
“Timu ya kuwezesha umwagiliaji (DIDT) District Irrigation Development Team ndiyo inapeleka mafunzo kuhusu umwagiliaji kwa wakulima ikishirikiana na wataalamu wa kanda” Alisema Mbowe
Amewataka wakulima kufanya shughuli za umwagiliaji katika utaratibu unaoeleweka ili ziweze kuwa endelevu.
“Umwagiliaji una gharama ,fedha zinazotakiwa hazifiki kwa wakati na kwa kiasi kinachotakiwa na hiyo ndio changamoto kubwa inayoikabili miradi mingi ya umwagiliaji hapa nchini” Alisema Afisa huyo
No comments:
Post a Comment