HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 05, 2013

Wabunge wasipowajibika kwa wananchi watasuswa!

Na Bryceson Mathias

WANANCHI kwenye Majimbo ya Uchaguzi, sasa wameanza kupata uelewa wa haki zao dhidi ya wabunge wao, jambo ambalo kama wasipowajibika kikamilifu kutetea haki zao, wana hatari ya kususwa.

Ni ukweli ulio wazi, kila Mbunge atapimwa kwa yale aliyoahidi jimboni kwake iwapo kama  ameyatekeleza asilimia ngapi. Lakini sina uhakika ni nani anatembelea majimboni ili kuuliza wapiga kura kuhusu utekelezaji  wa wabune wao.

Umahiri wa Mbunge katika jimbo lolote nchini ni kutatua kero za wananchi wake wala si kubwabwaja bungeni ili kuonekana kituko kwenye hadhara ya ulingo huo.

Ni kweli baadhi ya wabunge wengi ni mzigo tena mzigo mkubwa sana wengi tunawaona, wanaweza wasichangie chochote tangu bunge linaanza hadi linamalizika, labda tu utamsikia wakati wa kupiga kura anaposema ndiyooo!
 
Mbaya zaidi wabunge wengi utawakuta kila siku wako Bongo (DSM), hivyo unajiuliza hawana majimbo yao? Unajiuliza Je ni lini wanakuwa majimboni mwao kutatua kero za wapiga kura na wananchi wao?
 
Hivi karibuni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta aliwajia juu baadhi ya wabunge wa Chama chake (CCM) akidai kuwa ni mizigo kwani hata wakienda bungeni, hawachangii na wanabebwa tuu na Chama.

Sitta ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tisa, alisema hayo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Shule ya Msingi Nyamikoma, Kata ya Busega Mkoa wa Simiyu ikiwa ni sehemu ya kampeni za kuimarisha uhai wa CCM.

Alisema “Ukweli ni baadhi ya wabunge wa jinsi hii hawatufai. Wanakwenda bungeni hawachangii, wanakwenda bungeni hawana hata hoja za kuchachafya upinzani, hawachangii, hawa ni mzigo,” alisema Sitta.

Sitta aliongeza, aina hiyo ya wabunge, pia wapo wale ambao hawafiki majimboni kwao kukagua shughuli za maendeleo.

“Wapo ambao hawajawahi hata siku moja kwenda majimboni mwao kuwatembelea wananchi waliowachagua... inawezekana hata wapiga kura wakawa wamewasahau. Hawa hawafai hata kuchaguliwa wakiomba tena kura,” alisema Sitta.

“Haiwezekani Mbunge akakaa mjini na kushindwa kwenda kuwatembelea watu wake jimboni. Mbunge anakwenda jimboni kwa kuchungulia, halafu wananchi wanamshabikia na kumpa kura?

Alidai, “Rais Jakaya Kikwete amejitahidi kuleta mabadiliko, ameleta mafanikio ya uchumi. Inatakiwa wabunge waende wakawaeleze wananchi maendeleo haya, inawezekana hawayajui lakini hawaendi majimboni, wananchi watayafahamu vipi hayo maendeleo?”

Hivi karibuni uelewa wa namna hiyo, ulidaiwa kusababisha Mbunge wa Karagwe, Gozbert Blandes (CCM), ashindwe kufanya mkutano wa hadhara katika mji wa Kayanga, baada ya kukosa wananchi wa kuwahutubia, kwa kile walichodai alichakachuwa ushindi huo akitumia Dola.

Ilifahamika Blandes alipanga kufanya mkutano wa hadhara mjini Kayanga Jumamosi ya Agosti 3, 2013, lakini alilazimika kuuahirisha kwa sababu ya mahudhurio ya wananchi kuwa hafifu.

Mwandishi George Maziku, ni mmoja wa wana habari ambaye alituhabarisha kuhusu dalili za mkutano huo kutofanikiwa zilizoonekana siku moja kabla wakati mtu aliyekuwa akitangaza taarifa za kuwepo kwa mkutano huo aliposema; 

“Wale waliokuwa wakisema Blandes hawezi kufanya mkutano Kayanga waje wajionee.”

Katibu wa CCM wilayani humo, Anatory Nshange, alidai kuwa Blandes asingefanya mkutano huo kutokana na kuwepo kwa shughuli ya bomoa bomoa ya nyumba mbili za wananchi wa Chadema katika eneo la Mgakorongo. 

Matukioa hayo yanaonesha wananchi wana uelewa na Wabunge wasipowajibika kwa wananchi watasuswa! Kama alivyofanyiwa Blandes. Ingawa alikanusha!

nyeregete@yahoo.co.uk 0715-933308
 
NB: Picha ya Kikwete

No comments:

Post a Comment

Pages