HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 06, 2013

TFF: RUKSA TIMU YA 3 PILLARS KUCHEZA MECHI ZA KIRAFIKI TANZANIA

 Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura (Picha Na Maktaba).

DAR ES SALAAM, Tanzania

“FA ya Lagos imekiri kuiidhinishia ziara ya Pillars nchini, mchakato uliotokana na mawasiliano baina ya FA ya jimbo hilo ambayo ilikiri kufanya makosa ya kutowasilisha taarifa kwa NFF ambayo ina mamlaka ya kubariki ziara nje ya nchi”

TIMU ya 3 Pillars FC ya Nigeria, ambayo ilizuiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kucheza mechi za kirafiki nchini, sasa imeruhusiwa kucheza mechi hizo, baada ya TFF kupata idhini ya kutambuliwa na shirikisho la mchezo huo la Nigeria (NFF).

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo asubuhi, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alisema kuwa, Awali TFF iliikatalia timu hiyo kucheza mechi za kirafiki nchini kwa vile haikuwa na barua ya utambulisho kutoka NFF.

Aliongeza kuwa, sasa Shirikisho hilo limetoa idhini hiyo baada ya kuthibitiwa na NFF kuitambua ziara yao, iliyofanyika kutokana na kibali cha Chama cha Soka Jimbo la Lagos na sio cha NFF.

“FA ya Lagos imekiri kuiidhinishia ziara ya Pillars nchini, mchakato uliotokana na mawasiliano baina ya FA ya jimbo hilo ambayo ilikiri kufanya makosa ya kutowasilisha taarifa kwa NFF ambayo ina mamlaka ya kubariki ziara nje ya nchi,” alisema Wambura.

Sababu nyingine iliyokailazimisha TFF kutoitambua timu hiyo na ziara yake, ni ukweli kuwa haikuwa inaratibiwa na wakala wa mechi anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), au mwanachama wa shirikisho la mchezo huo nchini (TFF).

Kwa mujibu wa Wambura, 3 Pillars sasa inaweza kucheza mechi nchini, kwani licha ya kutambuliwa na NFF, lakini pia ziara hiyo sasa iko chini ya uratibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), ambaye ni mwanachama wa TFF.

Wambura alisisitiza kuwa, watu pekee wanaotakiwa kuandaa mechi za kirafiki za kimataifa ni mawakala wa mechi wanaotambuliwa na FIFA au wanachama wa TFF, hivyo kuwataka wadau kuachana na uratibu usiotambuliwa kisheria.

No comments:

Post a Comment

Pages