Na Salum Mkandemba
BARAZA la Vyama vya Soka kwa nchi za Afrika Mashariki na
Kati (CECAFA), limetuma salamu za pole na rambirambi kwa Mwenyekiti wa Shirikisho
la Soka la Kenya (KFF), Sam Nyamweya, huku likilaani shambulizi la kigaidi
lililotokea katika Kituo cha Biashara cha Westgate, jijini Nairobi mwishoni mwa
wiki.
Kwa mujibu wa taarifa ya baraza hilo iliyosainiwa na
Mwenyekiti wake, Leodeger Tenga, Cecafa na familia ya wapenda soka Afrika
Mashariki na Kati imejaa simanzi na huzuni kutokana na tukio hilo la kigaidi
lililoua makumi ya watu na kujeruhi zaidi ya watu 170.
Tenga ambaye pia ni Rais wa Shrikisho la Soka Tanzania
(TFF), amebainisha katika taarifa yake hiyo kuwa, wadau wa soka wa ukanda huu, wako
pamoja na Wakenya na wahanga wengine kwa tukio lililowapata na kuua na kujeruhi
watu wasio na hatia.
“Jumuiya ya wapenda soka imesikitishwa na tukio hilo
lililochukua uhai wa watu wasio na hatia, huku likiwajeruhi kadhaa. Tunatoa
ujumbe wa pole na rambirambi kwa wote waliopoteza ndugu na marafiki katika tukio
hilo la kikatili,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilienda mbali zaidi na kuwatakia majeruhi
ahueni ya haraka, ili waweze kurejea na kuungana tena na ndugu, jamaa na
marafiki zao katika ujenzi wa taifa, ikiwamo kuendeleza ushirikiano wao wa kila
siku.
Cecafa imesisitiza kuwa, itasimama wakati wote na KFF na
Wakenya kwa ujumla na kwamba baraza hilo lina uhakika kwamba litakuwa pamoja katika
vita ya kupambana na ugaidi, huku likiwaomba Wakenya kuwa na nguvu katika
kipindi hiki cha majonzi.
Jumamosi iliyopita, Kituo cha Biashara cha Westgate
kilichoko jijini Nairobi kilivamiwa na kundi la magaidi wa Al Shabaab la nchini
Somalia, na kushambulia wafanyakazi na wateja wa maduka yaliyo ndani ya jengo
hilo la ghorofa tatu.
Katika tukio hilo, zaidi ya watu 60 walifariki dunia, na
wengine zaidi 170 kujeruhiwa, huku wengine wakihofiwa kufunikwa na kifusi cha
jengo lililoporomoka kutokana na mashambulizi baina ya magaidi hao na vikosi
vya Majeshi ya Ulinzi ya Kenya na nchi washirika.
No comments:
Post a Comment