September 27, 2013

CECAFA YALAANI UGAIDI WESTGATE

Na Salum Mkandemba

BARAZA la Vyama vya Soka kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), limetuma salamu za pole na rambirambi kwa Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka la Kenya (KFF), Sam Nyamweya, huku likilaani shambulizi la kigaidi lililotokea katika Kituo cha Biashara cha Westgate, jijini Nairobi mwishoni mwa wiki.

Kwa mujibu wa taarifa ya baraza hilo iliyosainiwa na Mwenyekiti wake, Leodeger Tenga, Cecafa na familia ya wapenda soka Afrika Mashariki na Kati imejaa simanzi na huzuni kutokana na tukio hilo la kigaidi lililoua makumi ya watu na kujeruhi zaidi ya watu 170.

Tenga ambaye pia ni Rais wa Shrikisho la Soka Tanzania (TFF), amebainisha katika taarifa yake hiyo kuwa, wadau wa soka wa ukanda huu, wako pamoja na Wakenya na wahanga wengine kwa tukio lililowapata na kuua na kujeruhi watu wasio na hatia.

“Jumuiya ya wapenda soka imesikitishwa na tukio hilo lililochukua uhai wa watu wasio na hatia, huku likiwajeruhi kadhaa. Tunatoa ujumbe wa pole na rambirambi kwa wote waliopoteza ndugu na marafiki katika tukio hilo la kikatili,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilienda mbali zaidi na kuwatakia majeruhi ahueni ya haraka, ili waweze kurejea na kuungana tena na ndugu, jamaa na marafiki zao katika ujenzi wa taifa, ikiwamo kuendeleza ushirikiano wao wa kila siku.

Cecafa imesisitiza kuwa, itasimama wakati wote na KFF na Wakenya kwa ujumla na kwamba baraza hilo lina uhakika kwamba litakuwa pamoja katika vita ya kupambana na ugaidi, huku likiwaomba Wakenya kuwa na nguvu katika kipindi hiki cha majonzi.

Jumamosi iliyopita, Kituo cha Biashara cha Westgate kilichoko jijini Nairobi kilivamiwa na kundi la magaidi wa Al Shabaab la nchini Somalia, na kushambulia wafanyakazi na wateja wa maduka yaliyo ndani ya jengo hilo la ghorofa tatu.

Katika tukio hilo, zaidi ya watu 60 walifariki dunia, na wengine zaidi 170 kujeruhiwa, huku wengine wakihofiwa kufunikwa na kifusi cha jengo lililoporomoka kutokana na mashambulizi baina ya magaidi hao na vikosi vya Majeshi ya Ulinzi ya Kenya na nchi washirika.

No comments:

Post a Comment

Pages