Na Bryceson Mathias
NI mara kadhaa nimekuwa nikiandika na sasa naandika tena kuhusu tabia na vyanzo vya vurugu za wabunge zinazojirudiarudia kwa kuamshwa Naibu Spika Job Ndugai (CCM) hadi kutafsirika kuwa anakitumia kiti cha Spika ndivyo sivyo.
Katika vurugu nyingi zilizojiri siku za nyuma Ndugai akiwa kwenye Kiti hicho, tumeshuhudia Wabunge wakifyatua matusi ya nguoni na ambayo kwa Kiongozi ambaye ana familia inayomtegemea katika maisha yake hawezi kuthubutu kuyatamka ili kulinda heshima yake.
Ni siku chache nilikuwa nafanya utafiti iwapo kuna ukweli kufuatia malalamiko ya Ndugai katika Mkutano wa 12 Kikao cha 2 mwezi huu, alipowalalamikia wananchi wa Jimbo la Kongwa akidai kwamba, hawamuenzi hata kwa kumbukumbu za uzinduzi wa miradi jimboni mwake.
Ndugai alilalamika bungeni kuwa, hakuna Vyoo, Majengo, Shule, Zahanati, Miundo Mbinu ya Maji, Umeme na barabara ambazo hajashiriki kuziwezesha. Llakini wananchi wa jimbo lake waliohojiwa kwa nyakati tofauti walipinga vikali wakidai wanamtenga kwa sababu si mtoaji.
Mwananchi mwingine wa Pandambili ambaye naye aliomba asitajwe gazetini alieleza kwa ushahidi sababu zinazomfanya Ndugai asuswe hata asiwekwe au kuombwa kwenye uzinduzi wa kumbukumbu za Miradi jimboni mwake.
Alisema, kwa mfano wao wakulima na wajasiriamali wa Pandambili, wanalima alizeti nyingi na kukamua mafuta, lakini utaona wamepanga mafuta barabarani (Pandambili) kila baada ya hatua tano toka nyumba hadi nyumba, kama hawana Mbunge wa kuwatafutia masoko.
Meya wa Halmashauri ya Musoma, Alex Kasurura (Chadema), aliwahi kumkaanga Ndugai kwa wananchi wake 26.4.2013 katika Mkutano wa mabadiliko (M4C,) uliofanyika kata ya Pandambili na Kijiji cha Hembahemba Kata ya Njoge akisema,
“Pamoja na kujigamba kwenda nchi nyingi za Nje, bado Ndugai ameshindwa kuwatafutia Soko la Mahindi na Mafuta ya Alizeti wananchi wake Kibaigwa, bali anachoweza ni Ubabe wa kusababisha vurugu bungeni akiwafukuza wabunge wanaowatetea hata wananchi wake”.alisema Kasurura.
Nataka kuuliza ni nani asiyejitakia mema, akimuona Simba kashika Mnyama kwa ajili ya kitweo chake, anayeweza kuthubutu kwenda kumnyang;anya? Hata watanzania, hawawezi kukubali kuona Rais wao, Jakaya Kikwete, anafanyiwa chochote hadharani wakakaa kimya hata wawe wapinzani.
Kitendo cha Ndugai kuamuru Askari wa Bunge (Sergeant Arms) wamtoe, Freeman Mbowe, Kiongozi wa kambi ya Upinzani bungeni nje kwa kumkamata, ni sawa na kuwatukana au kuwadharirisha hadharani.
Hali hiyo kwa vyovyote vile, ndiyo iliyopelekea kutokea yaliyotokea hata kama kungekuweko mapungufu yoyote yaliyojiri, lakini katika hilo wasingekubali, na ndiyo maana yalitokea hayo tuliyoyaona bungeni ambapo hata CUF waliunga mkono.
Kimsingi uongozi si mabavu, Uongozi ni kipaji cha kuzaliwa nacho ambacho mtu hupata tangu tumboni mwa mama yake ambacho Yeremia katika Biblia 1:4-5 anasema,
“Neno la Bwana lilinijia, kusema, Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa”.
Je ni Mtoto gani ambaye ataona Mama yake anapigwa na Baba yake asiyeamka amtetee? Haya ndiyo mambo ambayo Ndugai anatakiwa kuyapa tafakuri kubwa anapokaa kwenye kiti cha Spika ambacho anayempa Jeuri ipo siku nyingine atamgeuka.
Siumi maneno, bado nasema na nitaendelea kusema kwamba, Tukimchekea Ndugai,aendelee kufanya yale anayoyafanya penye kiti cha Spika bila kuangalia kilicho mbele yake ipo siku atalipeleka taifa hili Pabaya, na tutalaumiana na kukumbuka tunayosema!
Ndiyo maana madereva barabarani huwa makini kutambua Nyoka, Paka na Mbwa.
nyeregete@yahoo.co.uk 0715933308
No comments:
Post a Comment