HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 01, 2014

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar afungua msikiti wa Kijiji cha Tasani Makunduchi

  Maustadhi wa baadae wakifurahia ufunguzi wa Madrasa yao ya Shafiiyat iliyopo Tasani Makunduchi uliofanywa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
 Ustaadhati Halima Rajab Hassan akimkabidhi zawadi ya kofia ya asili ya kiua iliyoshonwa Makunduchi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa niaba ya Rais wa Zanzibar mara baada ya kufungua Madrasa ya Shafiiyat ya Tasani Makunduchi.
 Balozi Seif kwa niaba ya Rais wa Zanzibar akiufungua rasmi Msikiti wa Kijiji cha Kajengwa utakaotoa huduma za ibada za sala na madrasa kwa waumini wa Kijiji hicho.
Balozi Seif akiwapongeza akina mama wa Kijiji cha Kajengwa kwa ushirikiano wao na Viongozi wao na hatimae kupelekea kupata nyumba ya ibada. 
      
Na Othman Khamis Ame,  OMPR – ZNZ.
                      
Wanazuoni, Masheikh na wazee wote nchini wana wajibu mkubwa wa kuisaidia Serikali Kuu katika jitihada zake za kukuza elimu, kujenga jamii iliyo bora, kulinda amani pamoja na kukataza maovu vikiwemo vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wa kijinsia.

Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Al – hajj Dr. Ali Mohamed Shein wakati akiufunguwa msikiti wa Kijiji cha Tasani  Makunduchi unaokadiriwa kusaliwa na waumini wapatao 200 kwa wakati mmoja wa sala.

Dr. Shein ambae Hotuba yake ilisomwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema katika msaada huo Masheikh wana fursa nzuri ya kuzungumza na waumini wao hasa kupitia hotuba za sala za ijumaa ili kujenga jamii iliyo bora.

Alisema Dini imekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa zaidi kwenye suala zima la kukuza maadili mema , malezi ya watoto sambamba na kuendeleza hali ya kuishi kwa upendo miongoni mwa jamii  yote.

Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Serikali imedhamiria kutilia mkazo mfumo wa Utawala bora unaozingatia utii wa sheria na kuendeleza mikakati katika kuimarisha uwajibikaji kwa kupiga vita ubadhirifu wa mali za umma.

Alifahamisha kwamba uimarishwaji wa mafunzo ya dini katika misikiti na hata madrasa una mchango mkubwa katika kuisaidia Serikali kuimarisha lengo lake hilo la usimamizi wa Utawala bora pamoja na utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

Al Hajj Dr. Ali Mohamed Shein amewapongeza Waumini na Wananachi wa Makunduchi kwa jitihada zao walizochukuwa na hatimae kufanikiwa kupata nyumba mpya ya Ibada.

Alisema Jamii imekuwa  ikushuhudia ongezeko kubwa la ujenzi wa misikiti mikubwa yenye nyenzo za kisasa katika pembe zote za Visiwa vya Unguja na Pemba neema ambayo Mwenyezi Muungu anaendelea kuishusha ndani ya Nchi hii.

Alieleza kwamba ujenzi wa Misikiti mipya ni ishara ya kuendelea kwa imani na mapenzi baina ya waislamu pamoja na kuongezeka kwa nguvu za kiuchumi miongoni mwa wananchi.

Dr. Shein aliikumbusha jamii kujitokeza zaidi katika kuwekeza katika mambo ya kheri kama hili la ujenzi wa misikiti ili kujitengenezea maisha bora ya baadaye na kuachana haya ya duniani ambayo ni ya mpito.

“ Na simamisheni sala na mtoe zaka na mkatieni Mwenyezi Muungu sehemu njema (katika mali yeni iwe ndio zaka na sadaka) na kheir yoyote mnayoitanguliza kwa ajili ya nafsi yenumtaikuta kwa mwenyezi mungu imekuwa bora zaidi na ina thawabu kubwa sana “. Dr. Shein aliikariri suratul Muzzammil aya ya 20.

Alisema ni vyema kwa waliojaaliwa uwezo kuangalia maeneo wanayoishi namna bora ya kutoa sadaka inayoendelea katika kupitia usambazaji wa huduma zinazohitajika na jamii iliyowazunguuka.

Alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikitekeleza dhamira ya kuhakikisha kuwa wananchi wake wanapata huduma muhimu katika maeneo wanayoishi.

Hata hivyo alisema zipo sababu tofauti zinazochangia kwa kiasi kikubwa baadhi ya wananchi kuendelea kukosa huduma hizo muhimu kwa maendeleo yao ya kijamii ya kila siku.

Aliwapongeza waislamu wote waliochangia pamoja na kushiriki kwenye ujenzi wa msikiti huo juhudi ambazo lazima ziambatane na kuendelea kuutunza  msikiti huo ili uendelee kubakia katika haiba yake ya kupendeza.

Katika kuunga mkono juhudi za waumini hao Balozi Seif  Ali Iddi Binafsi aliahidi kusaidia pampu ya kusukumia maji katika msikiti huo mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa mnara wa tangi la maji.

Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa Niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alilifungua jengo la Madrasatul Shafiat liliopo katika Kijiji cha Kajengwa Makunduchi.

Akizungumza na waumini hao Dr. Shein alisema ufunguzi wa madrasa hiyo ni kielelezo cha jitihada za wananchi wa kajengwa kwa kushirikiana na viongozi wao katika kutilia maanani haja ya kuwapatia elimu ya dini watoto wao jambo ambalo limefaradhishwa na mwenyezi mungu.

Alisema elimu nizawadi na urithi bora kwa watoto ambao huwajenga kuwa na ucha mungu, kujua utu, kuheshimu haki za watu wenye  imani za dini nyengine sambamba na kumtukuza mola anayeteremsha neema kwa viumbe wote.

Alitoa wito kwa uongozi wa Madrasatul Shafiat kufanya juhudi za makusudi kuisajili Madrasa hiyo ili ifuate taratibu zilizopo pamoja na kutambulika rasmi kiserikali.

Alisema Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kupitia kitengo kinachosimamia elimu ya maandalizina madrasa huzisajili madrasa ili kuzitambua , kusimaia taaluma inayotolewa , kuzipatia misaada ya kitaaluma vikiwemo pia vifaa.

Katika juhudi za kuunga mkono waumini hao wa Kajengwa Makunduchi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohd Shein aliahidi kuchangia mafeni yote ya Madrasat Shafiiya, Meza ya Mwalimu, pamoja na Makabati ya Vitabu vya Madrasa hiyo.

Akisoma risala ya walimu na Wanafunzi hao wa Madrasat Shafiiya Mwalimu Abou Simai Mussa alisema madrasa hiyo yenye wanafunzi karibu 150 inatoa mafunzo ya elimu ya Dini na Dunia.

Mwalimu Abou alisema madrasa hiyo hivi sasa imekuwa chem chem. Kubwa ya utoaji wa walimu na masheikh mbao wamekuwa wakitoa mafunzo ya kuongoza ibada katika misikiti mbali mbali ya Jimbo la Makunduchi.

Alimpongeza Mwakilishi wa Jimbo la Makunduchi kwa jitihada zake za kuchangia ujenzi wa msikiti huo zilizofikia zaidi ya asilimia 99% ukigharimu zaidi ya shilingi Milioni 21.3.

Akitoa shukrani kwa niaba ya wananchi na waumini hao wa Jimbo la Makunduchi Mwakilishi wa Jimbo Hilo Al Hajj Haroun Ali Suleiman alisema Uongozi wa Jimbo hilo utaendelea kushirikiana na wananchi hao katika kuhakikisha kwamba kero zinazowakabili zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Al – Haroun alisema tatizo la huduma za maji safi na salama ambalo limekuwa kero kubwa kwa wananchi hao hasa katika eneo la ibada la Msikiti atalishughulikia kwa kushirikiana na viongozi wenzake wa jimbo hilo.

Mapema Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Ngwali aliwakumbusha waumini hao kwamba Madrasa lazima zitumiwe kwa juhudi zote katika kujenga hatma njema  ya dunia na sfari ya milele.

No comments:

Post a Comment

Pages