Askari wa doria (kushoto) akisaidiana na askari wa magereza
(kulia) kushusha mwili wa mtuhumiwa wa dawa za kulevya, Abdul Koroma (33) raia
wa Sierra Leone aliyepiwa risasi wakati akijaribu kutoroka katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo. (Na Mpiga Picha Wetu)
Na Mwandishi Wetu
MTUHUMIWA mmoja wa kesi ya dawa za kulevya, Abdul Koroma (33)
raia wa Sierra Leone amepigwa risasi na kufariki dunia wakati akijaribu
kutoroka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo ambalo ni la kwanza kutendeka mahakamani hapo,
lilitokea leo majira ya saa tatu asubuhi kabla ya mtuhumiwa huyo na wenzake kupandishwa
kizimbani kwa ajili ya kusikilizwa kwa kesi zao.
Mtuhumiwa huyo alipigwa risasi kabla ya kesi yake kuitwa
mbele ya Hakimu Mkazi Agustine Mbando aliyekuwa akisimamia shauri hilo, kwa
niaba ya Hakimu Mwenzake
Warialwande Lema.
Akizungumza tukio hilo, mmoja kati ya Askari wa usalama
katika mahakama, kwa masharti ya kutotajwa majina.
Alisema,
kabla ya kupigwa risasi marehemu huyo aliomba apelekwe chooni ili akajisaidie,
lakini baada ya kufika chooni alianza kuchana suruali yake ya ‘jeans’ na
kubakia nusu kisha akachukua vipande vya suruali hiyo na kujifunga kwenye
viganja vya mikono ili asijikate na chupa wakati wa kuruka ukuta.
Chanzo
hicho kilieleza kwamba, wakati askari huyo akiendelea kumsubiri atoke chooni,
mtuhumiwa huyo alikuwa tayari amesharuka ukuta huo na kutokea upande wa pili
kwa ajili ya kutoroka.
Askari
huyo aliendelea kusema kwamba, wakati mtuhumiwa huyo akiwa mbioni kutoroka,
mmoja kati ya askari aliyekuwa kwenye Mgahawa wa Mahakama, alianza kupaza sauti
kwamba geti lifungwe kwani kuna mtuhumiwa anatoroka.
“Baada
ya askari kupiga mayowe, ghafla yule mtuhumiwa alimvamia kalani mmoja na
kumdondosha chini, ndipo askari mmoja wa magereza akaanza kufyatua risasi
hewani ili mtuhumiwa asikimbie,”kilieleza chanzo.
“Zilipigwa
risasi mbili juu ili mtuhumiwa asimame, lakini alikuwa mbishi na akaendelea
kukimbia na ndipo akapalamia nondo za ukuta ili aweze kukimbia.
“Wakati
akiendele na jaribio hilo, ndipo askari huyo aliyepiga risasi hewani akaamua
kumfyatulia risasi moja ya kichwani kutokana na kuzidiwa nguvu na mtuhumiwa
huyo ambaye tayari alishafanikiwa kuruka nondo za ukuta wa mahakama,”alieleza
askari huyo.
Kwa
upande wake Wakili wa Serikali, Tumaini Kweka, alisema mshitakiwa huyo alikuwa
na mashitaka ya kuingia na madawa ya kulevya nchini ambapo alikamatwa tangu
Desemba 2, 2013 katika uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Mwalimu Nyerere na
madawa aina ya Cocaine yenye thamani ya sh. 61 milioni.
Mwili wa Koroma ambaye alikuwa akikabiliwa na Kesi yake
P121/2013 uliondolewa katika eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kupelekwa Katika Hospitali ya Taifa ya
Mhimbili.
No comments:
Post a Comment