Na Othman Khamis Ame
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanikiwa vyema katika uimarishaji wa mtandao wa Bara bara Mjini na Vijijini na kufikia kilomita elfu 1,235.52 Unguja na Pemba tokea kubadilisha mfumo wa ujenzi wa Bara bara hizo katika miaka ya 90.
Alisema mfumo huo wa ujenzi kwa upangaji mawe na kushindilia kwa mkono umebadilika na kuingia mfumo wa kisasa unaotumia kifusi na kumalizia kwa lami ya moto na baridi.
Balozi Seif alieleza hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bara bara ya Pili ya Amani hadi Mtoni { Mkapa Road } ikiwa ni mwanzoni mwa shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 51 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964 zilizoanza rasmi Tarehe 2 Januari 2015.
Alisema Serikali ilichukuwa jitihada za makusudi katika kuzijenga upya bara bara zake Mijini na Vijijini ambazo tayari zilikuwa zimeharibika vibaya licha ya kazi hiyo kukumbwa na vikwazo tofauti ikiwemo ufinyu wa upatikanaji wa fedha za ununuzi wa zana, vifaa pamoja na ulipaji fidia.
Balozi Seif alisema kukamilika kwa ujenzi wa bara bara ya Amani – Mtoni ni miongoni mwa hatua muhimu za kuimarisha miundombinu itayowarahisishia wananchi usafiri kwa kuzingatia kuwa bara bara ni kiunganishi kikubwa kinachotumiwa katika kusafirisha huduma muhimu za Kiuchumi na Kijamii.
“ Hizi zote ni juhudi zinazochukuliwa na Chama cha Mapinduzi katika kutekeleza Ilani yake ya Uchaguzi kwa vitendo katika kuhakikisha Nchi ina bara bara bora na za kisasa, hii yote ni katika kuwaletea maendeleo wananchi wetu “. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza watendaji wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano katika kusimamia ujenzi wa Bara bara mbali mbali hapa nchini ambapo wameweza kutekeleza vyema majukumu waliyopangiwa na Taifa.
Balozi Seif alieleza kwamba haiba na uzuri wa Bara bara unategemea hali ya matunzo ya bara bara husika. Hivyo aliwaomba wananchi na watumiaji wote kuzitunza bara bara wanazozitumia ili zidumu na kuendelea kutumika kwa kipindi kirefu.
Alitoa wito kwa madereva wote wa vyombo vya moto kutumia bara bara kwa uangalifu zaidi pamoja na kufuata alama za bara barani zilizowekwa wakati wakiendesha vyombo vyao ili kuepuka ajali za mara kwa mara ambazo zinaweza kuepukika.
Aliwaomba madereva hao kuachana na mtindo wa kuegesha gari mbovu zinazodondosha mafuta na kuharibu bara bara sambamba na kuwa waangalifu kwa gari hasa zile zinazobeba makontena zinazotumia mipira ya magongo yanayopelekea uharibifu mkubwa wa bara bara.
Balozi Seif pia aliwakumbusha madereva kwenda mwendo mzuri kama alama za bara bara zinavyoainisha ya mwendo wa kilomita 40 kwa saa na kuepuka bara bara hiyo kufanywamakaburi ya watu wanaotembea kwa miguu na wale wanaotumia vyombo vodogo vya ringi mbili.
Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundo mbinu na Mawasiliano Zanzibar Dr. Juma Malik Akil alisema ramani ya ujenzi wa bara bara ya Mtoni hadi Kiembe Samaki ilikuwepo tokea awamu ya kwanza.
Dr. Malik alisema hatua za ujenzi wa bara bara hiyo zilianza mapemba katika miaka ya 90 lakini zilikwama baada ya daraja lililojengwa kuunganisha bara bara hiyo ambalo tayari lilikuwa limeshamikika kuvunjika.
Alisema ujenzi wa bara bara ya Amani hadi Mtoni yenye urefu wa kilo mita 4 na upana wa mita nane kila njia mbili zilizokuwepo umekamilika kwa awamu zote mbili na utasaidia kuondoa kiu ya wakaazi wa maeneo hayo waliopata usumbufu wa usafiri kwa kipindi kirefu.
Alifahamisha kwamba wahandisi wa ujenzi wa bara bara hiyo kutoka Idara ya ujenzi na Utunzaji Bara bara { UUB } iliyopata ufadhili wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mfuko wa Bara bara Zanzibar kwa gharama ya zaidi ya Shilingi Bilioni Nne imetenga njia maalum ya watembeao kwa miguu.
Katibu mkuu huyo wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar alieleza kwamba Serikali tayari imeshajenga Bara bara zenye urefu wa Kilomita 704 kwa Unguja na Kilomita 531 kwa Pemba.
Dr. Malik alifafanua kwamba hadi sasa tayari Mkoa wa Mjini Magharibi umeshawekewa miundombinu mizuri ya bara bara kwa zaidi ya Kilomita 206 kati ya hizo Manispaa ya Mji pekee ina kilomita 68, wakati bara bara kuu zina urefu wa kilomita 332, Vijijini Kilomita 544 na zile za mashambani zimefikia kilomita 270.2.
Akimkaribisha mgeni rasmi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Mh. Juma Duni Haji alisema licha ya bara bara ya Mtoni Amani kusaidia kupunguza msongamano wa Bara bara kuu inayoingia Mjini lakini matumizi yake yameongezeka na kuifanya kuwa na harakati zaidi.
Waziri Juma Duni alieleza kwamba hatua za kulinda usalama wa wananchi itaimarishwa kufuatia msongamano huo uliobeba magari makubwa hasa yale ya mchanga na mizigo.
No comments:
Post a Comment