HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 06, 2015

TUZO ZA FILAMU TANZANIA 2015 SASA ZAINGIA KWENYE HATUA YA MWISHO!

Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania Simon Mwakifwamba (kulia) akielezea jambo kwa wana habari(hawapo pichani) wakati wa kutangaza walioingia katika hatua ya mwisho ya kushindania Tuzo za Filamu Tanzania leo jijini Dar es Salaam katika mkutano na wana habari uliofanyika katika hotel ya New Africa ya jijini Dar es Salaam, kulia kwake ni Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya tuzo hizo Caroline Gul na mmoja wa wadhani kutoka International Eye Hospital Dr. Recep Yujel..
Jaji mkuu katika mchakato wa mchujo Issa Mbura kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akitoa ufafanuzi wa vipengere 11 vilivyoainishwa kushindaniwa.
Ofisa Masoko kutoka EATV/EA Radio Happy Shame ambao ni moja ya wadhamini wa tuzo hizi akitoa neno kwa niaba ya wadhamini wa Tuzo za Filamu Tanzania.
Mwakilishi kutoka Push Mobile Bwana Ezekiel akielezea namna ya upigaji kura ili kupata washindi tuzo hizi kubwa nchini

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Shirikisho la filamu Tanzania pamoja na wadau na waandaji wa tuzo hizo, wameonyesha furaha kubwa kwa hatua waliyofikia hadi sasa. 

Tuzo za filamu Tanzania chini ya shirikisho la filamu ndizo Tuzo zenye hadhi ya juu kabisa katika tasnia hii.  Tuzo hizi zilizozinduliwa rasmi mwaka jana mwezi wa kumi na moja zimeonyesha mwamko mkubwa sana katika uchukuaji na urekeshaji wa fomu na hatimaye kufikia hatua hii ya kuwapata, NOMINEES.


Mchujo wa kinyang’anyiro cha Tuzo za Filamu Tanzania imekamilika baada ya kufanyiwa uchambuzi wa kina na jopo la majaji. Kuna vipengele kumi na tatu vilivyoainishwa kutolewa katika za mwaka huu.  Kumalizika kwa mchakato huu wa kwanza, unatoa fursa sasa kwa watanzania kushiriki katika hatua inayofuata ambayo ni upigaji wa kura. 


Akitoa ufafanuzi wa mchakato huo kwa wana habari Jaji mkuu Issa Mbura ambaye pia ni muhadhiri msaidizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema kuwa uchambuzi wa kujaji filamu zilizowasilishwa ulijikita katika kutazama, kuchunguza na kudadavua kwa kina fani na maudhui yaliyopo katika filamu husika na kupendekeza ili kupata washiriki watano kwa kila kipengele, yaani ‘NOMINEES’ cha tuzo itakayotolewa. 

Pia alitoa wito kwa wana tasnia kujivunia kazi zao na kujiamini na kuona kuwa wanastahili tuzo. Hii ni kuleta msukumo kwa wana tasnia ya filamu nchini kuwasilisha kazi zao kwa wingi kwa miaka ijayo. 


“Napenda kuwashukuru waandaaji wa tuzo hizi kwa kuniamini na kunipa fursa ya kuwa jaji mkuu katika tuzo hizi kubwa katika tasnia ya filamu nchini. Matarajio tulikua tuwe na tuzo 24 lakini kutokana na uwasilishaji tutakuwa na na tuzo 11 ambazo zitatolewa mwaka huu”. 

“Tuzo hizo ni Best Feature Film, Best Director, Best Actor (in Leading Role), Best Actor (in Supporting Role), Best Actress (in Leading Role), Best Actress (in Supporting Role), Best Comedian (Male/Female), Best Screenplay, Best Sound, Life Time Achievement na Tribute Award” alieleza bwana Mbura.


Naye Raisi wa Shirikisho la Filamu Simon Mwakifwamba aliwashukuru jopo la majaji kwa kazi nzuri na kubwa waliyoifanya ambayo italeta urahisi katika kupiga kura.
Alisema “Napenda kuwapongeza na kuwashukuru jopo la majaji wakiongozwa na jaji mkuu Bwana Mbura kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya ya kuainisha kwa kifupi na kutupa urahisi wa kuingia hatua inayofuata. Kutokana na uainishaji uliofanywa na majaji sasa ni wakati wa kuanza kupiga kura ambapo mashabiki watapata nafasi ya kupigia kura filamu au msanii wa filamu anayempenda. Upigaji wa kura utakua ni kwa muda wa mwezi mmoja na pazia hilo litafungwa mwanzoni mwa mwezi Mei ili kupisha hatua nyingine ya mwisho kuelekea katika utoaji wa tuzo.”  .


“Wito wangu kwa wapenzi wa tasnia hii na watanzania kwa ujumla waendelee kuwaunga mkono kwa kudhamini tuzo hizi kubwa nchini katika tasnia ya filamu na pia kwa mashabiki wote wa tasnia hii wapige kura kadiri wawezavyo ili kuwapa ushindi wa tuzo wasanii wanaowapenda na filamu zinazofanya vizuri katika vipengele mbalimbali,” aliongezea kwa msisitizo Bwana Mwakifwamba.


Bwana Mwakifamba pia alishukuru kamati ya waandaji wa tuzo hizo haswa kwa mwenyekiti wa tuzo hizi, Caroline Gul, kwa moyo wa kujitolea ili kufanikisha tuzo hizi.  Pia aliwashukuru kampuni zilizojitolea kwa namna moja au nyingine.  Shukrani za dhati zilipewa East Africa Radio na TV, Push mobile, International Eye Hospital, kampuni ya vifaa vya nyumbani Pinetech na TCRA.   

Hata hivyo aliomba kampuni na mashirika mbali mbali kuitikia wito na kujitokeza kudhamini tuzo hizi ambazo zitatoa nafasi kubwa kwao katika kutangaza bidhaa zao. Baada ya upigaji wa kura, majaji kutoka bodi ya filamu ya Jumuiya ya Africa Mashariki watawasili nchini ili kutoa tamko la mwisho kuhusu washindi.  Baada ya hapo tuzo zinatarajiwa kufanyika tarehe 23 ya mwezi Mei jijini Dar es Salaam.


Tuzo hizi zipo kwa uangalizi mkubwa wa Baraza la filamu Tanzania katika Wizara ya  habari, vijana, utamaduni na michezo kwa kutambua kukua kwa tasnia hii hapa nchini.

No comments:

Post a Comment

Pages