HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 23, 2015

Viongozi wa dini: Kikwete simamisha Muswada wa Habari

Na Bryceson Mathias, Dodoma


WAJUMBE 205 wa Kamati ya Maadili ya Amani na Haki ya Jamii ya Viongozi wa Dini nchini, wameitaka Serikali kusimamisha Muswada wa Uhuru wa Kupata Habari kujadiliwa bungeni kwa madai kuwa unawanyima haki Watanzania kupata habari na haukustahili kuibuliwa wakati wa Uchaguzi Mkuu.

Kamati hiyo imemuomba Rais Jakaya Kikwete, ikimtaka akumbuke kauli yake mwenyewe ya mwaka 2001 akihamasisha wadau wa habari, aliposema, kama wananchi watakosa habari ndani ya mfumo wetu nchini, watazitafuta nje.

Akikiri kuwa na kikao cha viongozi hao Dodoma, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kipentekoste Tanzania, William Mwamalanga, alisema mbali ya kumtaka Kikwete asitishe muswada huo, pia wanapinga njama zozote zilizojificha nyuma ya muswada huo.

Mbali ya kusema kuwa viongozi hao wanaunga mkono tamko la wanachama wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (MOAT) la kutaka muswada huo usiendelee kujadiliwa bungeni, Mwamalanga amedai, muswada huo kwa wadau ni kama ‘petroli kwenye moto’.

Katika kikao hicho waandishi hawakuruhusiwa kwa madai wataruhusiwa siku ya mwisho ambapo viongozi hao watataka umma katika siku ya nne uhabarishwe, ingawa  mwandishi wa habari hizi alifanikiwa kunasa kilichozungumzwa na viongozi hao  wa dini na kumhoji Askofu Mwamalanga kama ni kweli.

Miongoni mwa maazimio saba yaliyoazimiwa na masheikh na maaskofu hao ambao ni wajumbe kutoka kila mkoa, ni pamoja na kuupinga muswada huo na kuiunga mkono MOAT na wadau wa habari katika kilio chao.

Yaliyokuwemo ni: Uhuru wa habari si wa vyombo vya habari, waandishi na wamiliki pekee yao, bali ni wa wananchi, hivyo haikuwa haki kupelekwa bungeni wakati wa uchaguzi kwani ulitakiwa upitiwe na wenye ueledi ili usiwabinye wadau hao kupata habari.


Wamedai muswada huo utawafanya wadau wa habari na wananchi wawachukie wabunge wao, hasa kutokana na ukweli kwamba, mchango wa vyombo vya habari umechangia kwa asilimia 81 kufichua uhalifu wa rushwa, ufisadi na kuliletea taifa maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. 

Wamesema vyombo vya habari na wanahabari vimekuwa ndiyo sehemu pekee ya kimbilio la wananchi wanyonge katika kupata haki zao kwa haraka kuliko mihimili mingine yoyote, hivyo ni wajibu muswada huo urudishwe kwao ili wenye ueledi katika  taaluma hiyo waujadili.

Wamedai wanapinga njama zozote zilizojificha nyuma ya muswada huo, kwa kuwa kupelekwa kwa muswada huo kwa hati ya dharura kunadhihirisha kilichoko nyuma ya pazia hilo, na kama  umelenga kuwanyima wananchi taarifa za uchaguzi, basi wahusika wameweka petroli kwenye moto.

Aidha, mwisho walisema kuwa kuchezea tasnia ya habari na uhuru wake ni sawa na kuchezea petroli kwenye moto, hivyo wanamuomba Rais Kikwete kusitisha muswada huo na kuwasikiliza wadau wake, kwa sababu kuwaburuza ni kutowatendea haki, isipokuwa kuchochea vurugu.

No comments:

Post a Comment

Pages