HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 27, 2015

RAIS DK. JOHN MAGUFULI AMSIMAMISHA KAZI KAMISHNA MKUU WA TRA

 Dar es Salaam, Tanzania

RAIS, Dk John Magufuli ametangaza kumsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya mapato nchini (TRA), Rished Bade (pichani), ili kupisha uchunguzi wa ufisadi wa mapato uliobainika katika baadhi ya maeneo ikiwamo katika Mamlaka ya Bandari nchini (TPA).

Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es salaam, amesema kuwa Rais Dk Magufuli amechukua umauzi huo ikiwa ni hatua za uwajibikaji kwa Bade, kutokana na kubainika kwa udanganyifu mkubwa bandarini uliosababisha kupotea kwa zaidi ya shilingi bilioni 80.

Sefue alisema pamoja na bade wapo maofisa wengine wa juu ambao wamesimamishwa kazi kwa ajili ya kupisha uchunguzi huo, ambao pia ameamuru wasiruhusiwe kusafiri nje ya nchi hadi uchunguzi huo utakapokamilika.

Kutokana na harua hiyo, Rais amemteua Dk. Philip Mpango ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Tume ya Mipango kukaimu nafasi hiyo ya Kamishna Mkuu wa TRA na amewataka wafanyakazi wote wa mamlaka hiyo kutoa ushirikiano wa kutosha katika kipindi chote cha uchunguzi,” alisema.

Alisema hatua hiyo ni miongoni mwa hatua  nyingi zitakazochukuliwa baada ya Serikali kupata taarifa za kina zinazoonyesha namna ambavyo ukusanyaji wa mapato umekuwa ukihujumiwa katika maeneo mengi nchini, ambapo kwa upande wa bandari ya Dar es Salaam pekee imebainika ukwepaji mkubwa wa kodi unaofanywa na wafanyabiashara kwa kushirikiana na maofisa wa TRA.

Kutokana na hali hiyo, Sefue amesema kuwa Rais ameamuru wafayabiashara wote walioshiriki ukwepaji kodi na kuipotezea serikali mapato hali zaidi ya sh. Bilioni 80 wajitokeze kwa hiyari yao na kulipa fedha zote walizoiibia serikali.


Balozi Sefue aliongeza kuwa "Serikali imedhamiria kuhakikisha mapato yake yote yaliyopotea yanapatikana na kudhibiti mianya yote ya mapatio kuanzia sasa, akisisitiza kuwa kwa upande wa bandari kazi ndio imeanza na hakutakuwa na msalie mtume".

“Kuhusu kampuni ambazo kwa namna moja au nyingine zimeshiriki katika iukwepaji wa kodi na wizi wa mapato ya Serikali kisha kufilisika au kuondoka nchini, tutatumia nguvu ya kisheria kuwanasa wahusika waliokuwa wakizimiliki na kuziendesha ambao tuna uhakika tutawapata na tutawashughulikia kikamilifu,” alisema.

Alieleza kuwa hatua hiyo haitabagua, bali itawahusu wafanyabiashara wote waingizaji wa bidhaa na mizigo ambao wanajijua kwamba walishiriki katika mchezo wa aina hiyo, ambao kwa sasa wanatakiwa kujisalimisha na kulipa mapato yote ya serikali waliyoyakwepa kabla sheria haijachukua mkondo wake.

Wakati uchunguzi ukiendelea balozi Sefue amesema kuwa maofisa wote wa TRA waliohusika na upotevu huo wametakiwa kutosafiri nje ya nchi na kusalimisha hati zao za kusafiria.
Balozi Sefue akionesha majina ya makampuni yaliyokwepa kodi.

No comments:

Post a Comment

Pages