HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 14, 2015

Mhagama awataka watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kufanya kazi kwa Uzalendo

Taarifa kwa Vyombo vya Habari
  
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu na Bunge; Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Bibi Jenista Mhagama (Mb) amewataka wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wajitume zaidi ili kuendana na kasi ya Rais John Pombe Magufuli.

“Tunapaswa kuendana na kasi ya Hapa Kazi Tu. Tunatakiwa tuache kufanya kazi kwa mazoea na badala yake tufanye kazi kwa bidii tukiongozwa na moyo wa uzalendo,” amesema.

Ametoa wito huo wakati akizungumza na wakuu wa taasisi na idara pamoja na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu mara baada ya kuwasili ofisini kwake leo asubuhi (Jumatatu, Desemba 14, 2015) na kupokewa na watumishi hao wakiongozwa na Katibu Mkuu, Dk. Florens Turuka.

Bibi Mhagama alisema: “Tunapaswa tufanye mabadiliko ili kuendana na kasi ya Mheshimiwa Rais. Na kama ni utendaji kazi Serikalini, basi mabadiliko makubwa yanapaswa yaanzie katika ofisi hii,” alisema.

Waziri wa Nchi ambaye alikuwa ameambatana na manaibu wake, Dk. Possi Saleh Abdalla (Wenye Ulemavu) na Bw. Anthony Peter Mavunde (Kazi, Ajira na Vijana) alisema ana imani na manaibu hao kwani ni vijana na wachapakazi hodari. “Hawa ni wachapakazi, ni wazalendo na wanasheria waliobobea, sote tuna wajibu wa kumsaidia Mheshimiwa Rais kwa kuwatumikia wananchi,” alisema.

Pia alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Magufuli kwa imani aliyoonyesha kwao na kuwateua kushika nyadhifa hizo. “Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutuamini na kututeua. Tumepokea kwa mikono miwili uteuzi huu na tunaheshimu majukumu aliyotukabidhi,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Dk. Turuka akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu (OWM), aliahidi kutoa ushirikiano kwa mawaziri hao wakati wote na kwa kadri inavyowezekana.

Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Ofisi ya Waziri Mkuu
S. L.P 3021
Magogoni, Dar es Salaam
14 Desemba, 2015.

No comments:

Post a Comment

Pages