Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza katika mkutano wa mwaka wa mapitio ya sekta ya afya unaofanyika kwenye ukumbi wa Karimjee jijini Dar es salaam, wadau hao wa Sekta ya afya wanajadiliana mambo mbalimbali na baada ya kumalizika kwa mkutano huo kutakuwa na kusaini makubaliano yaliyofikiwa kwa utekelezaji katika sekta ya afya hapa nchini , Katika picha kulia ni Carol Hannon Mshauri wa Afya katika ubalozi wa Ireland nchini Tanzania. PICHA NA JOHN BUKUKU-FULLSHANGWE
Carol Hannon Mshauri wa Afya katika ubalozi wa Ireland nchini Tanzania akizungumza katika mkutano huo Kushoto ni Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu.
- KINGA NA AFYA YA JAMII
Mwaka 2015 Serikali ya Tanzania ilikamilisha Mpango wa Afya katika Jamii na kuanzisha mafunzo kwa kada mpya za Wahudumu wa Afya ya Jamii (Community Health Workers). Wafanyakazi hawa wana jukumu kubwa kuifikishia jamii huduma za afya za msingi.
Mwaka 2016, Serikali ya Tanzania itaendelea kutekeleza agenda ya huduma za Afya katika jamii kwa kuhakikisha ubora wa mafunzo kwa wahudumu wa Afya ya Jamii, kuendelea kuajiri wahudumu wa Afya ya Jamii na kufikisha huduma za Afya za Kinga na tiba karibu zaidi na jamii.
- UWIANO
Mpango Mkakati wa Nne wa Sekta ya Afya (HSSP IV) umejielekeza zaidi katika uwiano na kusaidia maboresho katika Sekta ya Afya katika maeneo ya pembezoni ambayo huduma za Afya hazifiki kwa urahisi. Jambo muhimu katika hili ni kuendelea kusambaza kwa uwiano rasilimali zote za kifedha zilizopo kutoka vyanzo vya ndani na nje.
Ili kuhakikisha uwiano katika mgawanyo wa rasilimali, ni muhimu kuwa na takwimu sahihi kuhusu uwepo wa rasilimali kutoka vyanzo vya nje hususan wadau wa maendeleo, sekta binafsi, mashirika ya dini na mashirika yasiyo ya kiserikali katika ngazi ya wilaya.
Serikali itahakikisha kwamba takwimu zilizopo zinaboreshwa kwa kukamilisha Mpango Kabambe wa kutambua vyanzo vya nje vya mapato kwa mwaka 2016.
- UGHARAMIAJI WA HUDUMA ZA AFYA
Mpango wa Afya kwa wote ni kipaumbele cha Serikali ya Tanzania. Mkakati mpya wa ugharamiaji wa Afya ulioandaliwa umeweka wazi njia ambayo Tanzania inaweza kutoa huduma za Afya za uhakika wa kifedha kwa raia wote kupitia mfumo mmoja wa Bima ya Afya ya Taifa.
Kwa mwaka 2016/2017, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto itatafuta kibali kutoka Mpango Mkakati wa ugharamiaji Afya na itaandaa hatua muhimu za utekelezaji wa Mkakati ikiwa ni pamoja na kuhamasisha kupitishwa kwa Sheria ya Mfuko Mmoja wa Kitaifa wa Bima ya Afya na kuleta pamoja mitazamo mbalimbali ya Mfuko wa Afya ya Jamii.
Vilevile, wizara itafanya uhamasishaji ili kuongeza rasilimali za ndani kwa ajili ya Sekta ya Afya na kuongeza jitihada za Wizara mbalimbali katika kuboresha matumizi yenye ufanisi wa rasilimali fedha zilizopo.
Wizara na Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa zitaunda Mfumo rahisi wa utoaji taarifa kuhusiana na mipango, bajeti na fehda, kwa ajili ya vituo vya utoaji huduma za afya, ili kuwezesha ugatuaji wa kifedha kutoka wilaya kwenda ngazi ya vituo vya afya.
- UTAWALA NA UONGOZI
Kuna miundo mbalimbali ya utawala na uwajibikaji ndani ya Serikali na katika jamii inayofanya kazi katika ngazi ya wilaya hususani katika masuala ya Afya kama vile Kamati za Uongozi za Vituo vya Afya na zile zenye mamlaka makubwa zaidi kama vile Kamati za Maendeleo za kata. Zote hizo zinajukumu la kuhakikisha uwajibikaji katika utoaji huduma za Afya kwa wananchi.
Kwa mwaka 2016 Wizara, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wadau wengine zitaweka wazi mahusiano kati ya miundo hii katika ngazi ya wilaya kuhusiana na Usimamizi wa Mipango, bajeti na fedha kwa ajili ya Afya. Vilevile ili kuendeleza agenda ya ugatuaji, Wizara itashirikiana na Wizara ya Fedha kusimamia mgawanyo wa fedha katika ngazi ya vituo vya kutolea huduma za Afya.
- RASILIMALIWATU KATIKA SEKTA YA AFYA.
Kuvutia na kuwezesha idadi kubwa ya watumishi kuendelea na kazi katika utoaji huduma bora za Afya hususan katika maeneo ya vijiji na maeneo ambayo huduma za Afya hazifiki kwa urahisi, ni changamoto nchini Tanzania, maendeleo ya kuridhisha yamefanyika kupitia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa na Program nyingine.
Ili kuendeleza zaidi mafanikio yaliyofikiwa, mwaka 2016 Wizara, Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa zitaendeleza Sera ya mabadiliko yanayohitajika ili kutekeleza mpango wa mabadiliko makubwa sasa (BRN) kuhusiana na rasilimali watu katika nyanja za afya na zitashirikiana na Serikali za Mitaa kuwezesha utekelezaji wa Sera ya Malipo na motisha.
Ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya, Wizara itakamilisha mwongozo wa kushirikiana katika majukumu, kuweka wazi majukumu ya kila kada na kukamilisha mwongozo wa kujiendeleza kitaaluma.
- DAWA, VIFAA NA VIFAA TIBA
Uboreshaji wa usimamizi na utawala wa Dawa, vifaa na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya hususan katika ngazi ya wilaya ni kipaumbele chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa na Mpango wa Nne wa HSSP.
Matatizo ya kifedha yana maanisha kwamba rasilimali zilizopo hazina budi kutumiwa kwa ufanisi na namna nyingine za ugharamiaji wa dawa na vifaa vingine muhimu hazinabudi kutafutwa. Ili kuhakikisha haya yanafanyika, mwaka 2016 Wizara itajielekeza katika kuboresha utendaji na ufanisi wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ikiwa ni pamoja na kuwezesha ulipaji wa deni.
Kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara vilevile itahakikisha rasilimali zilizopo na nyingine mpya kwa ajili ya usambazaji wa vifaa zitaelekezwa katika vipaumbele vya mpango wa Matokeo Makubwa Sasa na itatoa miongozo sahihi ya Kisera inayoainisha Mfumo mmoja wa ununuzi wa dawa na vifaa tiba muhimu itakayofuatwa na mamlaka ya Serikali za Mitaa na vituo vya kutolea huduma za Afya.
- UFUATILIAJI, TATHMINI NA USIMAMIZI WA TAKWIMU
Maboresho mengi yamefanywa katika mfumo wa usimamizi wa takwimu kwenye Sekta katika miaka ya hivi karibuni, hata hivyo bado kuna changamoto hususan kwa upande wa uhamiaji kwenda katika Mfumo wa kielektroniki na matumizi ya takwimu katika utoaji wa matumizi.
Uwepo wa takwimu sahihi utasaidia wilaya kupanga vizuri matumizi yao.
Wizara imedhamiria kukamilisha Mpango wa kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya huduma za afya kufikia mwisho wa mwaka 2016, ikiwa ni pamoja na kuhama kutoka mfumo wa kutumia karatasi kwenda mfumo wa kielektroniki na pia katika kuongeza uwezekano wa kuunganisha mifumo ya takwimu.
Ili kuendeleza dhana ya utoaji uamuzi unaotokana na ushahidi, Wizara itashirikiana na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika masuala ya takwimu muhimu zinazotokana na mamlaka za Serikali za Mitaa na watumiaji wengine kwa wakati katika mfuko rafiki unaowezesha utoaji wa taarifa za mipango na utoaji wa maamuzi.
- UTOAJI HUDUMA
Mwaka 2015 Wizara ilianzisha Mfumo wa tathmini wa vituo vya msingi vya utoaji huduma za afya.
Mfumo nyota ambao unazingatia vigezo vya ubora wa huduma (quality of service) za madaraja katika kuanzisha viwango vya utoaji huduma. Mwaka 2016 Wizara kwa ushirikiano na TAMISEMI itahakikisha kwamba tathmini ya Matokeo ya nyota inatafsiriwa katika uboreshaji huduma katika vituo na kwamba ugharamiaji unawekwa katika Mpango Kabambe wa Afya wa kituo na Halmashauri. Mfumo nyota unaonyesha vituo katika kazi mkoa, rufaa na Taifa utakamilika 2018.
Vilevile, Wizara itaipitia miongozo iliyopo ya usimamizi ili kuainisha majukumu ya ukaguzi na usimamizi.
UZINDUZI WA MPANGO MKAKATI WA NNE WA SEKTA YA AFYA 2015-2020
Utangulizi
Mpango mkakati wa nne (HSSPIV) ni mpango ulioandaliwa kwa kuwashirikisha wadau wote wa sekta ya Afya ikiwa ni pamoja na Serikali, Wadau wa Maendeleo, Sekta binafsi, taasisi za kijamii na Ustawi wa jamii.
Lengo kuu la mpango huu ni :kufikisha huduma bora muhimu za Afya na Ustawi wa jamii katika ngazi za kaya zote nchini.
Mpango unaainisha Mikakati mitano:
1.Kuboresha kiwango cha Ubora wa huduma katika ngazi zote za afya ya msingi kwa kuhakikisha kuwa kila mwananchi anafikiwa na kitita bora cha afya na ustawi wa jamii
- Kuboresha Uwiano wa upatikanaji wa huduma bora za afya na ustawi wa jamii kwa kuondoa tofauti zilizopo za kijografia, kiuchumi na makundi maalum kama vile wazee, watoto, wajawazito na walemavu.
- Kuboresha Ushirikishwaji wa jamii katika kupanga na kusimamia huduma za Afya na Ustawi wa jamii. Hii inajumuisha uhamasishaji wa mifuko ya afya ya jamii, usimamiaji wa vituo vya huduma, uwepo wa dawa vituoni, utambuzi wa wasiojiweza ili wapate huduma, na uwajibikaji wa watoa huduma kwa wanajamii husika.
4.Uwekezaji katika mikakati na njia za kisasa na ubunifu
kama : Ugharamiaji
-Mkakati wa Bima moja ya Afya kwa wote
-Ushirikiano na sekta binafsi
-Ushirikiano wa wadau wote wa sekta ya afya maendeleo na ustawi wajamii.
5.Kutambua Ushiriki wa jamii na Sekta nyingine katika afya. Afya bora siojukumu la wizara moja; Hii inajumuisha uhamasishaji wa wa kila sekta kuwa na mkakati wa Afya.
Hii itasaidia kushughulikia mambo muhimu kama; Lishe na afya za watoto, Maji safi, elimu ya afya, Usafi wa mazingira, umuhimu wa barabara na mawasiliano katika dharura ya kiafya na itapunguza magonjwa kama kipindupindu, vitambi, presha
No comments:
Post a Comment