Na Talib Ussi, Zanzibar
CHAMA cha waandishi wa habari Wanawake Tanzania upande wa Zanzibar (TAMWA) kimemuomba Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein kuangalia usawa wa kijinsia wakati wa uteuzi wa viongozi mbali mbali katika serikali.
Tamwa kilieleza kimepata wasiwasi kuona nafasi za juu katika serikali yake zinaelekezwa kwa wanaume pekeyao baada ya kuona Uteuzi wa Makamu wa Pili na Pomoja uchaguzi wa Spika.
Kwa mujibu wa taarifa ya TAMWA kwa vyombo vya habari iliotolewa na Mratibu wa chama hicho Mzuri Issa imeeleza kuwa wanawake wamekuwa wakiachwa nyuma katika maeneo mengi ikiwemo siasa, uchumi na kijamii.
Mzuri kupitia taarifa hiyo alifahamisha kuwa vipindi vilivyopita nafasi za wanawake katika Baraza la Mawaziri na nafasi za uteuzi wa Rais pia hazikuwa nyingi kulinganisha na wenzao na hivyo kuendelea kuwa na pengo la usawa wa kijinsia.
“Hivyo TAMWA Tunamuomba Rais ukumbuke kuwa usawa wa kijinsia ni kipaumbele katika mipango mbali mbali ya nchi na ulimwengu ikiwemo ya Malengo ya Uendelezaji wa Maendeleo (SDGs) pamoja Mpango wa Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA)” alieleza mzuri kupitia tarifa hiyo.
Alisema kupitia taarifa hiyo kwamba katika Serikali Rais iliyopita aliteua mawaziri 4 wanawake kati ya 19 wakiwa ni sawa na asilimia 21 wakati awali walianza na nafasi mbili na katika nafasi za uteuzi kwa nafasi 10 za Rais, wanawake walikuwa ni 4 hadi mwisho sawa na asilimia 40.
Taarifa hiyo iliendelea kwa kueleza kuwa Kukosekana kwa usawa wa kijinsia katika vyombo vya maamuzi pia kunarejesha nyuma maendeleo ya nchi kiuchumi na kielimu hasa kwa vile wanawake ndiyo wanawakilisha zaidi ya asilimia 50 ya wananchi wote.
Wanahakati mara kwa mara wamekuwa wakipiga kelele killa siku suala la usawa kijinsia katika nafasi za kutoa maamuzi pamoja na zile kuongoza nchi.
Haijawahi kutokea Zanzibar kuwa na Rais, Makamu, Spika au Katibu mkuu kiongozi kutoka Jinsia ya kikee licha ya sauti kupaa za wanaharakati duniani kote kupitia mikutano na makongamano mbali mbali.
No comments:
Post a Comment