HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 04, 2016

CUF: Hatumtambui Shein kama rais Zanzibar

CUF
Image captionChama cha CUF kilisusia uchaguzi wa marudio
Chama kikuu cha upinzani visiwani Zanzibar kimesema hakimtambui Dkt Mohamed Ali Shein aliyetangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa marudio uliofanyika mwezi uliopita.
Viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF), wakizungumza kwa mara ya kwanza tangu kufanyika kwa uchaguzi huo ambao chama hicho kilisusia, wamesema hawamtambui Dkt Shein kama rais wa visiwa hivyo.
“Tangu mapema, tangu Jecha (Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Jecha Salim Jecha) alipofuta uchaguzi, tulisema waziwazi kwamba haikuwa halalali. Walipoitisha uchaguzi wa marudio, tulisema waziwazi uchaguzi huo sisi hatuutambui na tukawataka wananchi wasipige kura,” amesema Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad.
Bw Hamad alikuwa mgombea urais wa chama hicho katika uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba mwaka jana na ambao matokeo yake yalifutwa na tume.
“Kama Rais ametokana na mchakato ambao hamkuutambua nyinyi tangu mwanzo, sasa leo kuja kusema hatumtambui kwa nini iwe ni haramu? Hatumtambui.”
Chama hicho kimesema kitatumia njia za kidemkrasia kulalamika dhidi ya Dkt Shein na serikali yake.
Aidha, kimeiomba jamii ya kimataifa kuwawekea vikwazo watu binafsi waliofanikisha uchaguzi huo wa marudio ambao chama hicho kimesema ulikuwa “uongozi haramu”.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama Twaha Taslima amesema chama hicho hakiko tayari kuwa sehemu ya serikali mpya.
"CUF haitoshirikiana na serikali itakayoundwa kwa sababu ni kinyume na katiba ya Zanzibar, kinyume na sheria ya uchaguzi na haikutokana na ridhaa ya watu," amesema.
Wiki iliyopita, Shirika la Changamoto za Milenia la Marekani (MCC) lilisitisha ufadhili wa $472milioni kwa Tanzania likilalamikia uchaguzi visiwani Zanzibar na utekelezwaji wa Sheria ya Uhalifu wa Mtandao.
Pesa hizo zilikuwa za kutumiwa katika miradi ya kusambaza umeme.
CUF imesema upo uwezekano wa kurudiwa kwa uchaguzi visiwani humo ka ikiwa uchaguzi huo utarudiwa basi usimamiwe na ujumbe wa kimataifa kwani wasimamizi wa ndani wamepoteza uhalali
Chama tawala visiwani humo kimebeza tamko hilo la CUF ana kusema kuwa Wazanzibari ni watu makini na kwamba hawawezi kumnyima ushirikiano Rais wao ambaye anafanya kazi kuwaletea maendeleo
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai ameiambia BBC kwamba Rais Shein anao pia uwezo wa kutengeneza serikali hata bila ushiriki wa chama cha CUF
"CUF wanafanya upotoshaji. Katiba haijamfunga Rais kukamilisha utengenezaji wa serikali yake. Na hivi tunapozungumza, muda si mrefu atakamilisha serikali yake na atajumuisha Wazanzibari na kufanya nao kazi" alisema Vuai.
Hii ni mara ya kwanza kwa Chama cha CUF kutoa tamko tangu kurudiwa kwa uchaguzi ambao waliususia. BBC

No comments:

Post a Comment

Pages