Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MKUU wa mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana amesema
hajawahi kumsikia Mh. Rais John Magufuli
kuzuia michezo ya Mei Mosi, ambayo ilianza Aprili 18 mwaka huu kwenye viwanja
vya Jamhuri mkoani Dodoma.
Katika hotuba yake ya uzinduzi wa michezo hiyo
iliyosomwa juzi na Afisa Maendeleo Vijana, Tumsifu Mwasambale kwa niaba yake,
alisema ameshangazwa na idadi ndogo ya timu shiriki, huku nyingi zikitoa
kisingizio kuwa Mh. Rais amekataza michezo hii, ambayo kauli mbiu yake ni ‘Hapa
kazi tu isiwe kisingizio kwa waajiri kuondoa michezo kazini’.
“Nashangaa sana kwani nimesikia kuwa timu nyingi, ambazo
zilikuwa ndio washiriki wakubwa hazijashiriki kwenye mashindano ya mwaka huu,
kwa viongozi wao kusingizia kuwa Mh. Rais amekataza, mimi sijasikia kuhusu hilo
kabisa,” alisema.
Alisema kuwa endapo Mh. Rais Magufuli angekuwa
amekataza michezo, asingemteuliwa Mh. Nape Nnauye kuwa Waziri wa Wizara ya
Habari, Vijana, Sanaa na Michezo, hivyo kuwataka viongozi mahala pa kazi kuacha
visingizio vya kumsingizia Rais wakati hajatoa tamko kuhusu hilo.
“Nasema huo ni uoga usiokuwa na mashiko, kwani hata
ingekuwa hivyo hata Mh. Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) asingekutana na viongozi
wa mashirikisho na vyama vya michezo kule uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, miezi
mitatu iliyopita kuzungumzia uimarishaji wa michezo, hivyo nawalaumu sana
viongozi waliowanyima haki wafanyakazi
wanamichezo kuja kushiriki kwenye michezo hii,” alisema Rugimbana.
Hatahivyo, alisema Mh. Rais Magufuli anachotaka ni
uhalisia wa yale yanayofanywa na viongozi wa serikali ni uhakika na kweli na
kusiwe na udanganyifu wowote.
Rugimbana alisema michezo mahala pa kazi inasaidia
kujenga na kuimarisha afya za wafanyakazi ili waendelee kutoa huduma bora iliyotukuka
kwa wananchi na kuongeza tija zaidi mahala pa kazi, pia husaidia kujenga
mahusiano mema ikiwa ni pamoja na kubadilishana mawazo.
Pia aliwataka wachezaji kucheza kwa nidhamu na
waache vitendo vya utovu wa nidhamu, kwani hatasita kuripoti kwa waajiri wao.
Awali Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mei Mosi,
Joyce Benjamin, naye katika hotuba ya ufunguzi aliwalaani viongozi wa mahala pa
kazi kumsingizia Mh. Rais kuwa amezuia michezo na kusababisha mashindano ya
mwaka huu kutokuwa na timu nyingi kama miaka ya nyuma.
Benjamin alisema kuwa hadi juzi ni timu 14 pekee
zilizofika mkoani hapa kushiriki kwenye mashindano haya, wakati nyingine
zikizuiwa na viongozi wao, bila kuwa na sababu za msingi.
“Kumbukeni Mh. Rais ni mmoja wa wanamichezo na ndio
maana hata wakati wa kampeni tulimuona wote akipiga pushapu jukwaani, sasa
iweje leo hii viongozi wa sehemu za kazi waseme amekataza michezo, michezo huu
ni mikubwa imepata Baraka zote kutoka TUCTA (Shirikisho la Vyama vya
Wafanyakazi) na Baraza la Michezo la Taifa (BMT),” alisema Benjamin.
Michuano hii inashirikisha michezo ya soka,
netiboli, kuvuta kamba, karata, bao, darts, riadha na mbio za baiskeli.
No comments:
Post a Comment