HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 11, 2024

Wakulima wapewa mbinu kutengeza pembejeo za asili

Na Mwandishi Wetu

WAKULIMA nchini wameshauri kutumia mashirika yanayohamasisha kilimo ikolojia hai, ili kujifunza mbinu za kutengeneza viuatilifu na mbolea kwa njia ya asili.

Ushauri huo umetolewa na wataalam wa kilimo ikolojia hai kutoka Shirika la Kilimo Endelevu Tanzania (SAT) na Kilimanjaro Permaculture Community (KPC), wakati wakizungumza na mwandishi wa habari hii.



Daudi Gwabara ni Meneja Miradi Msaidizi kutoka SAT alisema  kutengeneza viuatilifu na mbolea asili hauna gharama na ni salama kwa mkulima, ardhi na mazingira.

Alisema Tanzania ni moja ya nchi yenye rasilimali asili nyingi ambazo zikitumika vizuri kwenye kilimo, asilimia 100 ya mazao yatakuwa yamezalishwa kwa mfumo wa kilimo ikolojia hai ambao u akubalika duniani kote.

Gwabara alisema Shirika la SAT ambalo lipo mkoani Morogoro limewezesha zaidi ya wakulima 3,000 nchini kutumia mbinu za kilimo ikolojia hai na matokeo yake yamekuwa makubwa katika ubora wa mazao na soko la uhakika.

Alisema rasilimali za kilimo ikolojia hai zinapatikana shambani, hivyo ni rahisi kwa mkulima yoyote kuzitumia na kwea gharama ndogo. 

Gwabara alisema mchakato wa kutengeneza viautilifu vya asili unahitaji, molasesi lita mja, tangawazi kilo moja, kitunguu saumu kilo mbili, pilipili kali kilo mbili, konyagi chupa kubwa au pombe kali lita moja na vinega lita moja.

“Tunaposema dawa ya kudhibiti wadudu waharibifu ipo shambani ni katika muktadha huu, kwamba mkulima anaweza kununua molasesi lita moja, tangawizi kilo moja, kitunguu saumu kilo mbili, pilipili kali kilo mbili, konyagi kubwa na vinega lita moja vitu ambavyo mkulima yoyote anaweza kununua kwani gharama haizidi shilingi 50,000,” alisema.

Mtaalam huyo alisema baada ya kuchanganya vitu hivyo na kupata lita 16 hadi 20 mkulima anatakiwa kuchukua lita tatu hadi tano na kuchanganya na lita 100 ya maji ambapo ataweza kupulizia shamba lenye hekari 20 na kuendelea.

Gwabara alisema mchanganyiko huo ukikamilika unatambulika kama kiuatilifu kinachoitwa Apichi, hivyo kuwataka wakulima kutumia teknolojia hiyo ambayo ni rahisi.

“Inasikitisha sana mkulima anatumia gharama nyingi kununua dawa za viwandani, huku gharama ya kupuliza shamba la hekari 20 anaweza kutumia Apichi iliyogharimu shilingi 50,000, lazima tubadilike tupende vitu vya asili kwa teknolojia hii inalinda afya ya mkulima, mlaji, udongo na mazingira,” alisema.

Mtaalam huyo alisema matumizi ya teknolojia ya asili kwenye kilimo inachangia chakula kuwa na ladha nzuri, virutubisho na kuhakikishia usalama wa afya kwa watumiaji.

Gwabara alisema mchakato mzima wa kutengeneza kiuatilifu cha Apichi unahitaji siku tano, ili mkulima aweze utumia na mimea kuwa salama.

Akizungumzia mchakato wa utengenezaji wa mbolea ya asili, Gwabara alisema wanatengeneza kwa kutumia bidhaa ambazo ni rahisi kupatikana.

“Tunatengeneza mbolea yenye kirutubisho cha nitrojeni, tunatumia bidhaa zinazopatikana kwa mkulima kama matunda ya nanasi, papai lilokomaa na kuiva, molasesi na maziwa ambayo yametoka kukamuliwa kwa kuwa yana vitamini nyingi, kwani bakteria wanaoenda kuchachusha wanapata chakula,” alisema.

Alisema molasesi inatumika kama nyenzo ya kuongeza nguvu kwa bakteria kukuwa na kuzaliana kwa wingi.

Mtaalam huyo alisema mbolea hiyo inavunda baada ya kukaa siku 30 ambapo mkulima anaweza kutumia kuotoesha na kukuzia mazao.

Gwabara alisema lita tatu hadi tano ya mbolea hiyo inapaswa kuchanganywa kwenye lita 100 ya maji ambapo matumizi ni kila mmea kupata mbolea kiasi cha robo lita.

“Iwapo mkulima analima kilimo cha kitalu anaweza kuunganisha katika mfumo wa umwagiliaji wa dripu na kuweza kusambaza shamba nzima na mimea ikaweza kupata mbolea safi na salama,” alisema.

Alisema mazao kama mpunga mkulima naweza kutumia njia ya solo ambayo inaweza kusambaza kwa urahisi kwenye mimea yote ya jamii hiyo.

Mtaalam huyo alisema pia wanatengeza mbolea ya kukuzia mimea ambayo inaitwa Super Magro ainayotengenezwa kwa kutumia kinyesi, molasesi, maziwa na majivu ambayo yanasaidia kupunguza PH.

Alisema mbolea hiyo baada ya kutengenezwa inakaa siku 30 ndipo ianze kutumika kwa kuweka kila shina robo lita na mazao yataweza kukuwa kwa haraka bila shida yoyote.

Gwabara alisema teknolojia hiyo imepokelewa na wakulima katika Wilaya ya Kongwa, Morogoro, Chamwino, Mpwapwa, Dodoma, Simanjiro, Masasi, Karatu, Kigamboni, Mbaralim, Kilosa na baadhi ya wilaya za Mkoa wa Njombe na kwingine.

Alisema wadudu ambao ni viumbe hai wana manufaa katika kilimo, hivyo wanapaswa kukabiliwa na njia za asili ili kuhakikisha hawadhuriki.

“Ni katika muktadha huo sisi watu wa kilimo ikolojia hai tunasema dawa ya kukabiliana na wadudu wasumbufu au mazao kutokua kwa haraka ipo shambani na sio viwandani kama ambayo inahamasishwa kwa sasa,” alisema.

Alisema utafiti ambao wamefanya kwenye mashamba ambayo yalikuwa yakitumika kwa kilimo cha mbolea na viautilifu vya viwandani, baada ya kubalidilika na kutumia mfumo ya kilimo ikolojia hai mavuno yameongezeka mara dufu, huku ardhi ikiwa safi na salama.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa KPC, Frank Marwa alisema katika kilimo ikolojia hai wanatambua mbolea za aina tatu ambazo ni mbolea ya kupandia, kukuzia na yakunenepeshea mazao kama matunda.

“Mbolea ya kupandia tunatumia majaji ya kijani na kijivu, udongo wa porini wenye bakteria nyingi, mbolea ya mifugo ambapo mchanganyiko wake ukifanyika vizuri inatumika katika kilimo. Mbolea mboji ipo ya siku 14, 30, miezi mitatu, sita hadi mwaka,” alisema.

Marwa alisema pia wanatengeza mbolea asili inayotokana na mabaki ya gesi ya kinyesi cha ng’ombe.

Alisema mbolea hii baada ya gesi kuzalishwa, kipo kinyesi ambacho kinabaki, hivyo kikichakatwa kwa kufuata utaratibu na kupunguza ukali uliopo ili isiungeze mazao.

“Ipo mbolea inayokana na mabaki ya chakula kama karoti, nyanya, kitunguu na vinginevyo, ambayo inaandaliwa kwa kuweka kwenye chombo cha taka kama dumu ambalo unalitoboa na kuweka nyasi kavu na minyoo wekundu wanaozosha mbolea baada ya kuweka takataka.

Minyoo watakuwa wanameng’enya mabaki ya chakula, hivyo maji yakayotoka ndio yanafaa kwa mbolea,” alisema.

Marwa alisema mbolea hiyo inatumika mahususi kwa ajili ya kukuzia na kunenepesha matunda  kwa kuwa ina kiwango kukubwa cha potashiamu manganise, nitrojeni na kalishamu.

Alisema wanashauri wakulima kutumia mbolea hizo kwa kuwa zinauwezo mkubwa wa kukuza mazao, kutunza ardhi kwani ardhi hii tumeazimwa, mazingira na afya ya mlaji.

Pia Marwa alisema wametengeza teknolojia nyingine ya kuchuja maji taka na kutumika kwa ajili ya umwagiliaji, hivyo kuwataka wakulima wawatumie ili kupata elimu hiyo.

“Nyumbani kwetu tunazalisha maji taka, hivyo tumekuja na teknolojia ambayo inatumia ndoo na kuweka mawe na majaji ambayo yanachuja maji hayo na kuweza kumwagilia nyumbani bila gharama kubwa. Na mfumo huu unaweza kutumika katika mazingira ambayo hayana maji ya kutosha," alisema.

Naye Mkulima Abdi Kiduka kutoka Wilaya ya Chemba alisema teknolojia hiyo ambayo inatumia rasilimali zinazopatikana shambani inapaswa kuungwa mkono ili kuhakikisha wakulima wazalishaji mazao bora na salama kwa mlaji.

Kiduka alisema serikali inahitajika kushirikishiana na wadau wa kilimo ikolojia hai kuhakikisha kundi kubwa la wakulima linafikiwa kwa haraka, ili kuweza kutengeneza kizazi bora.

Mkulima wa Kilimo Ikolojia Hai kutoka MVIWAMORO, Tatu Magongo alisema mbinu ya kuandaa kiuatilifu chenye sumu kwa njia asili inapaswa kufikia wakulima wengi.

Magongo alisema amekuwa akilima kwa nia za kilimo ikolojia hai kwa muda mrefu hivyo ni wakati wa kuendeleza taaluma hiyo kwa wakulima wenzake.


No comments:

Post a Comment

Pages