Na Mwandishi Wetu, Dodoma
TIMU ya Uchukuzi SC iliyopo chini ya Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, imeibuka kinara kwenye mashindano ya Mei Mosi
baada ya kutwaa vikombe 11 vya michezo mbalimbali.
Timu hiyo imetwaa ubingwa katika michezo ya netiboli,
baiskeli na bao (wanaume), kamba
(wanawake na wanaume); huku vikombe vya ushindi wa pili ni vya michezo ya bao
(wanawake) na draft (wanaume); wakati vya ushindi wa ni katika soka, karata
(wanaume), riadha (wanawake na wanaume).
Hatahivyo, kutokana na uwingi wa vikombe timu hiyo
inatarajia kutangazwa mshindi wa jumla kesho kwenye sherehe za Mei Mosi na
kukabidhiwa kombe na Mh. Rais John Magufuli.
Timu nyingine na idadi ya vikombe zilizopata ni Tamisemi
saba kikiwemo cha ubingwa wa soka baada ya kuwafunga GGM katika fainali kwa
magoli 2-0, huku TPDC wakiwa na vikombe vitano sawa na Tanesco.
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), wamejikusanyia vikombe
vinne, Ujenzi vikombe viwili, na Mawasiliano, Ukaguzi na Halmashauri ya Nyasa kila mmoja wana
kikombe kimoja kila mmoja.
Awali katika michezo iliyochezwa jana timu ya
Uchukuzi SC iliwafunga Tamisemi kwa magoli 18-15 katika mchezo wa netiboli,
ambapo wafungaji wake Tatu Kitula na Matalena Mhagama waliwapeleka puta wapinzani
wao na hadi mapumziko walikuwa mbele kwa magoli 11-7.
Washindi wote walikabidhiwa kombe na mgeni rasmi
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (TRAWU), Mussa Kalala, ambaye
katika hotuba yake aliwashutumu viongozi
walioshindwa kupeleka timu zao kwenye mashindano hayo na kusema michezo mahala
pa kazi husaidia kuijenga miili ya wafanyakazi kuendelea kuwa mikakamavu na
kuwa na afya bora, ambapo hutoa huduma bora iliyotukuka na kuzalisha tija
zaidi.
Naye Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya mashindano
ya Mei Mosi, Joyce Benjamin alisema wamesikitishwa na ushiriki wa timu chache mwaka
huu, ambazo ni 11 pekee ukilinganisha na mwaka jana zilikuwa 28.
“Pamoja na kamati yetu kusikitika kwa uchache wa
timu zilizoshiriki katika michezo ya mwaka huu, hata mkuu wa mkoa katika hotuba
yake ya uzinduzi wa michezo hii naye alisikitika ambapo wote kwa pamoja tumesikitishwa sana na viongozi wengi
kutoleta timu zao hatujii kwa sababu ya kumuogopa Mh. Rais pengine kwanza labda
amekataza michezo, au wana sababu zingine tu zao binafsi,” alisema Benjamin.
Mwanaisha Athuman wa Uchukuzi SC akipokea kombe la ubingwa wa netiboli kutoka
kwa mgeni rasmi Mwenyekiti TRAWU, Mussa Kalala, katika mashindano ya Mei Mosi.
Wachezaji wa Uchukuzi SC wakiwa wamevipanga vikombe 11 walivyotwaa kwenye michezo mbalimbali ya Mei Mosi, iliyomalizika juzi mkoani Dodoma.
Bingwa wa baiskeli Chaptele Muhumba wa Uchukuzi SC akiwa amekumbatia kombe alilotwaa kwenye mashindano ya Mei Mosi.
Wachezaji na viongozi wa Uchukuzi SC wakishangilia baada ya kufanya vizuri kwenye mashindano ya Mei Mosi yaliyomalizika juzi mkoani Dodoma.
No comments:
Post a Comment