HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 06, 2016

ASKOFU NZIGIRWA AWAFUNDA VIONGOZI NCHINI

Na Mwandishi Wetu

VIONGOZI na watendaji katika ngazi mbalimbali, wametakiwa kufanya kazi na majukumu yao kwa kuzingatia ukweli na uadilifu.

Akihubiri katika Ibada ya Misa ya sherehe ya Kupaa kwa Yesu kristo, iliyofanyika juzi katika Kanisa Kuu la Mt Joseph Jijini Dar es Salaam, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Askofu Eusebius Nzigirwa, alisema taifa litasonga mbele ikiwa watendaji waliopewa madaraka watasimamia ukweli hata ikiwalazimu kupoteza maisha yao.

Mhashamu Nzingirwa katika Ibada ya Misa hiyo, ambayo iliendana sambamba na  kumwombea Rais John Pombe Magufuli ambaye Mei 5, mwaka huu ametimiza miezi sita tangu ashike madaraka,  alisema taifa litasimama imara na kuwa na maendeleo ikiwa viongozi na watendaji wake watatenda na kutimiza majukumu yao kwa kuzingatia uadilifu.

“Ikiwa umepewa madaraka ya kusimamia jambo au wajibu fulani, ni lazima ufanye kazi hiyo kwa uaminifu mkubwa, na usikubali kudanganywa kwa namna yoyote kusudi ukiuke kile unachopaswa kutenda.

“Tabia iliyozuka ya kupiga “dili” na kuona kama ni haki yako, sio tu itaangamiza taifa, lakini inaleta hasara kwako kiroho kwa sababu ni kwenda kinyume na amri za Mungu na imani yako uliyoiungama” alisema.

Askofu Nzigira aliongeza kuwa, watendaji na watumishi wengi walipopewa dhamana sehemu mbalimbali, wanaogopa kusema au kusimamia ukweli kwa hofu ya kuchukiwa na wakubwa au marafiki zao, na hivyo wako tayari kupotoka na kutenda kinyume na viapo vyao vya kazi.

“Mitume wa Yesu wote kasoro mmoja, waliuawa kwa sababu walisema na kusimamia ukweli. Hawakuogopa mtu kwa sababu ni mkubwa ama mdogo bali ukweli” alisema na kuongeza kuwa, ni heri kwa mtumishi wa serikali au taasisi afukuzwe kazi kwa kukemea na kuzuia uovu, kuliko kuendelea kuchuma dhambi itakayomwangamiza milele.

Aliwataka watendaji na watumishi wa kila sekta kutumia nafasi zao kwa uangalifu, uadilifu na kujali zaidi haki na maslahi ya wengine.
 Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Askofu Eusebius Nzigirwa akizungumza kwenye Ibada ya Misa ya sherehe ya Kupaa kwa Yesu kristo, iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam juzi. (Picha na Francis Dande) 
Baadhi ya waumini wakiwa katika ibada hiyo.

No comments:

Post a Comment

Pages