Mwenyekiti wa kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge Mhe.George Huruma Mkuchika akiwasilisha taarifa ya Kamati hiyo kuhusu uchunguzi es vitendo vya baadhi ya wabunge kufanya vurugu.
Na Aron Msigwa-Dodoma
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge limepitisha azimio la kuwasimamisha kuhudhuria vikao vya Bunge
baadhi ya wabunge wa Kambi ya Upinzani waliohusika katika kufanya vitendo vya
vurugu ndani ya ukumbi na kudharau Mamlaka ya Spika Januari, 27, 2016.
Wabunge waliosimamishwa kuhudhuria vikao hivyo ni Mhe.Kabwe Zubeiri Ruyangwa
Kabwe, Mhe.John Heche, Mhe.Halima Mdee,Mhe.Tundu Lissu, Mhe.Halima Mdee,
Mhe.Pauline Gekul na Mhe. Ester Bulaya.
Azimio la adhabu
kwa wabunge hao limetolewa na Bunge chini ya Kifungu cha 30A (1) cha sheria ya
Haki Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 na kanuni ya 74 (4) na (6).
Akisoma adhabu hizo Mwenyekiti wa kamati hiyo yenye
wajumbe 15 Mhe.George Huruma Mkuchika amesema kuwa uchunguzi uliofanywa na
Kamati hiyo kwa kuwaita na kuwahoji wahusika ulibaini kuwa wabunge hao walitenda kosa kwa kukiuka kanuni zinazoliongoza bunge hilo.
Imebainishwa kuwa Mhe.Zitto Kabwe
alivunja masharti ya Kifungu cha 24(c), (d) na (e) cha Sheria ya Haki na Kinga
na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 na Kanuni ya 60(2) na (12) , 74(1) na (b) kwa
kusimama na kuzungumza bila kufuata utaratibu na kudharau mamlaka ya Spika.
Kamati hiyo ilibaini kuwa Mhe.Godbless Lema, Mbunge wa
Arusha alivunja Masharti ya kifungu cha 24 (c),(d) na (e) cha Sheria ya Haki,
Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 pamoja na Kanuni ya 74(1) (a) na (b) ya
kanun hiyo Kudharau Mamlaka ya Spika.
Kwa upande wa Mhe.John Heche alivunja
kanuni ya 72 (1) na 68(10) ya kanuni za Bunge kwa kuendelea kusimama na kuomba
mwongozo kwa jambo ambalo limekwishatolewa mwongozo na kuongeza kuwa vitendo
hivyo vilivuruga shughuli za Bunge.
Kwa mujibu wa maelezo ya kamati hiyo Mhe.Halima Mdee, Mhe.Tundu Lissu,Mhe
Pauline Gekul na Mhe.Ester Bulaya
walivunja masharti ya kifungu cha 24 (c), (d) na (e) cha sheria ya Haki,Kinga
na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 na Kanuni ya 72 (1)68 (10), 60(2) na 12 na
74(1) (a) na (b) kwa kusimama na kuendelea kuomba mwongozo kwa jambo ambalo
limekwishatolewa uamuzi, kuzungumza bila kufuata utaratibu na kudharau Mamlaka
ya Spika.
Kufuatia uchunguzi huo Bunge kupitia kamati hiyo
limeazimia kuwa Mhe. Ester Bulaya na Mhe.Tundu Lisu wasihudhurie vikao vyote
vya mkutano wa tatu wa Bunge la Kumi na Moja vilivyobaki kuanzia tarehe 30 Mei
, 2016 pamoja na vikao vyote vya Mkutano wa Nne wa Bunge la Kumi na Moja kwa
kuwa walipatikana na makosa ya ukiukwaji wa Kanuni na kuonyesha dharau kubwa
kwa mamlaka ya Spika.
Aidha, Bunge limeazimia kuwa Mhe. Pauline Gekul,
Mhe.Godbless Lema, Mhe.Zitto Kabwe na Mhe Halima Mdee wasihudhurie vikao vyote
vya mkutano wa tatu wa Bunge kuanzia tarehe 30 Mei 2016.
adhabu hizo
Bunge limeazimia Mhe.John Heche asihudhurie vikao kumi mfululizo vya Mkutano wa
Tatu wa Bunge hilo kuanzia Mei, 30, 2016 kwa kuwa alipatikana na kosa moja na
pia kwa kuwa alitoa ushirikiano kwa kamati kwa kufika na kujibu maswali yote
kama alivyoulizwa pamoja na kuheshimu vikao vya kamati na Mwenyekiti
aliyeongoza vikao hivyo.
Pamoja na adhabu hizo Kamati hiyo imetoa maoni na
mapendekezo kuwa Bunge liandae mafunzo ya kutosha kwa wabunge wote kuhusu
matumizi ya uzingatiaji sahihi wa kanuni sahihi wa kanuni za Kudumu za Bunge
hasa kanuni za majadiliano ndani ya Bungeni.
Aidha, Kamati hiyo imesema kuwa ipo haja ya kutungwa
kwa kanuni za maadili kwa wabunge wote kama kifungu cha 12 A Cha Sheria ya
Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge kinavyoelekeza ili kuweza kudhibiti nidhamu
kwa wabunge kwa kuhakikisha heshima na hadhi ya Bunge inadumishwa.
Kwa upande wao baadhi ya wabunge wakichangia kwa
nyakati tofauti kuhusu suala hilo wamesema kuwa ipo haja ya Bunge kurudisha
heshima yake kwa wabunge wote kuheshimiana na kutoa michango yenye staha kwa
kuzingatia nafasi walizonazo katika jamii.
Wamesema kuwa michango wanayoitoa ndani ya Bunge hilo
lazima ijikite katika masuala yanayowahusu wananchi wanaowawakilisha badala ya
mambo yanayochochea vurugu na kulifanya Bunge lipoteze heshima yake katika
jamii.
Aidha, wabunge hao wamekubali kwa kauli moja kuanza
upya kuzingatia kanuni zinazoendesha vikao vya Bunge huku wakimtaka Spika wa
Bunge au Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kutosita kuchukua hatua
za haraka kwa mbunge yeyote atakayekiuka utaratibu na kanuni zilizowekwa.
No comments:
Post a Comment