Michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) msimu wa 2015/2016 inaendelea vizuri katika vituo vinne vya Kagera, Morogoro, Singida na Njombe ambapo itafikia tamati Juni 6 mwaka huu.
Timu sita zitapanda daraja kucheza Ligi Daraja la Pili (SDL) msimu wa 2016/2017. Timu hizo ni zile zitakazoongoza kila kundi, na washindwa bora (best losers) wawili kutoka makundi mawili tofauti.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeweka waangalizi wake katika kila kituo, na litawachukulia hatua watu wote watakaobainika kutumia michuano hiyo kuchafua viongozi.
Mtwivila City ya Iringa inaongoza kituo cha Njombe ikiwa na pointi sita baada ya kucheza mechi tatu. Katika kituo hicho kesho (Mei 31) kutakuwa na mechi kati ya Jangwani FC ya Rukwa na Nyundo FC ya Katavi kwenye Uwanja wa Amani.
Timu inayoongoza kituo cha Morogoro ni Namungo FC ya Lindi yenye pointi saba kwa mechi tatu. Kesho (Mei 31) ni mechi kati ya Makumbusho FC na Sifapolitan, zote za Dar es Salaam itakayofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Kitayose ya Kilimanjaro inaongoza kituo cha Singida ikiwa na pointi tisa baada ya kushinda mechi zote tatu ilizocheza. Kesho (Mei 31) kwenye kituo hicho kutakuwa na mechi kati ya Stand FC ya Tabora na Murusgamba ya Kagera itakayochezwa Uwanja wa Namfua.
Mpaka sasa vinara wa Kituo cha Kagera ambacho mechi zake zinachezwa Uwanja wa Vijana mjini Muleba ni Mashujaa FC ya Kigoma yenye pointi saba.
No comments:
Post a Comment