HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 13, 2016

TANZANIA YATAKIWA KUSHIRIKI MKUTANO WA UWEKEZAJI NORWAY

WAZIRI MKUU wa Norway, Bibi Erna Solberg amemuomba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ahakikishe Tanzania inatuma wawakilishi wa Serikali kwenye mkutano wa uwekezaji unaopanga kujadili fursa za uwekezaji barani Afrika utakaofanyika jijini Oslo, Norway, Oktoba mwaka huu.

Bibi Solberg ametoa kauli hiyo jana (Alhamisi, Mei 12, 2016) alipokutana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kufanya naye mazungumzo ya ana kwa ana kwenye mkutano wa siku moja wa Wakuu wa Nchi ulioitishwa kujadili suala la kupambana na rushwa duniani.

Akizungumzia kuhusu mkutano huo, Waziri Mkuu wa Norway alisema mkutano huo umeandaliwa na taasisi binafsi ya Norway Africa Business Association (NABA) na kwamba anazo taarifa kuwa utalenga kujadili fursa za uwekezaji barani lakini focus ikiwa ni Tanzania.

“Ni vema Tanzania ikatuma wawakilishi kwenye mkutano ili waje kuelezea fursa zilizoko nyumbani. Serikali ilete watu wa kuja kuelezea hali halisi ikoje nchini Tanzania,” alisema.

Alisema ili fursa za uwekeaji ziweze kutumika ipasavyo, ni vema Tanzania ikawa na mfumo wa kimahakama unatoa haki bila upendeleo (a fair judicial system) kwani utasaidia kujenga hali ya kujiamini kwa wafanyabiasha wanaokuja kuwekeza Tanzania.

“Mfumo huu utaleta hamasa kwa wawekezaji, kwani watajua kwamba mitaji yao iko salama na inalindwa kisheria, hivyo hawatakuwa na hofu,” alisema.

“Hata hivyo, napenda kusisitiza kuwa makampuni yanayotoka nje na kuja kuwekeza Tanzania hayana budi kuheshimu sheria za nchi yenu pamoja na za huku wanakotoka,” alisisitiza.

Akijibu hoja hiyo, Waziri Mkuu alisema usawa wa kisheria upo nchini kwa sababu Tanzania imesaini mikataba ya kimataifa ya MIGA na ICSID (International Centre for Settlement of Investment Disputes) ambayo inahusika na usuluhishi wa migogoro ya kibiashara.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa alimweleza Bibi Solberg kuwa Tanzania inahitaji kujifunza kutoka Norway katika suala la uanzishwaji wa mfuko wa Sovereign Wealth Fund ili mapato yatokanayo na rasilmali za nchi yatunzwe kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Naye akaipongeza Serikali ya awamu kwa kuanzisha wazo la kutaka kuanzisha mfuko huo hata kabla ya kuanza kuuza rasilmali hizo. Pia alimtihibitishia Waziri Mkuu kuwa wao wako tayari kubadilishana uzoefu na Tanzania katika suala hilo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
IJUMAA, MEI 13, 2016.

No comments:

Post a Comment

Pages