HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 28, 2016

Wazee Yanga waomba kadi mbili uchaguzi Yanga

 Katibu wa Baraza la Wazee wa Klabu ya Yanga, Ibrahim Akilimali akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya klabu hiyo jijini Dar es Salaam.  Kulia ni mjumbe wa baraza hilo, Abdallah Kibavu na Athuman Kaungu. (Picha na Francis Dande)
Na Mwandishi Wetu

BARAZA la Wazee wa Klabu ya Yanga, limelipigia magoti Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuwaomba kuwaruhusu wanachama wa timu hiyo kupiga kura kwa kutumia kadi zote za zamani na zile za Benki ya Posta.

Ijumaa Mei 27, Kamati ya Uchaguzi ya TFF, chini ya Wakili Aloyce Komba, ilianza rasmi mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Yanga, ulioitishwa na BMT, ikitaka ufanyike kwa kadi za zamani, kupigia kura za kuwateua viongozi wapya baada ya waliopo kumaliza muda.

Akizungumza Makao Mkuu ya klabu hiyo, mitaa ya Twiga na Jangwani leo, Katibu wa Baraza la Wazee Yanga, Ibrahim Akilimali, aliliomba BMT na TFF kutengua uamuzi wao wa awali wa kutaka kura zipigwe kwa kadi za zamani, kwani utawatenga baadhi ya wanachama.

Amefafanua kwamba, busara inapaswa kutumika katika mchakato huo, kwani wamiliki wa kadi za sasa walizibadilisha kutoka zile za zamani, hivyo kuwabagua ni kutowatemndea haki na kuwanyima haki ya msingi ya kuchagua na kuchaguliwa kuiongoza Yanga.

“Sisi kama wazee tunapata shaka ya kuwepo kwa uwezekano wa vurugu na mgogoro mkubwa Yanga, utakaosababishwa na agizo hilo la BMT na TFF. Ikumbukwe kuwa wenye kasdi hizi walibadilisha kihalali na wanazilipia kwa miaka miwili sasa,” alisema Akilimali.

Ameongeza kuwa, hiyo haitakuwa mara ya kwanza kwa Yanga kufanya uchaguzi kwa kutumia kadi mbili tofauti, kwani iliwahi kufanya hivyo mwaka 2006, wanachama walipopiga kura wakitumia kadi za Yanga Kampuni na Yanga Asili.

Mzee Akilimali alienda mbali na kuziomba taasisi hizo kubwa katika uratibu na uendesha wa michezo nchini, kuiruhusu Sekretarieti ya Yanga kuitisha Mkutano wa Dharura wa Wanachama, wenye ajenda moja ya kutoa elimu juu ya kadi kuelekea uchaguzi.

Amebainisha kuwa, Mkutano wa Dharura hautaathiri mchakato wa uchaguzi, kwani utaitishwa na kufanyika wakati Kamati ya Uchaguzi ya TFF ikiendelea na mchakato wake kama ilivyopanga na wameomba hivyo kutokana na kutotambuliwa kwa uongozi Yanga.

“BMT na TFF hawautambui uongozi Yanga, hivyo kuondoa uhalali wa iliyokuwa Kamati ya Uchaguzi, tunakubaliana na hilo na tuko tayari kuwa chini ya Kamati ya Wakili Komba, ndio mana tunaomba haki ya kuitishwa mkutano wa dharura ipewe Sekretarieti,” alisema.



No comments:

Post a Comment

Pages