Kikosi cha Serengeti Boys.
Na Mwandishi Wetu
KIKOSI cha timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 ya
Tanzania 'Serengeti Boys' imetinga raundi ya pili ya michuano ya kuwania kufuzu
fainali za Mataifa Afrika (2017 AFCON U-17), baada ya kuwachapa Shelisheli kwa
mabao 6-0.
Kwa ushindi huo, Serengeti Boys inayonolewa na Bakari
Shime 'Mchawi Mweusi', imefuzu raundi ya pili ya michuano hiyo, ambako itaumana
na Afrika Kusini, baada ya kuing'oa Shelisheli kwa ushindi wa jumla wa mabao
9-0, hii ni baada ya kushinda mechi ya kwanza kwa 3-0.
Serengeti Boys ililianza pambano hilo kwenye Uwanja wa Stade
de Linate mjini Victoria kwa usongo na iliwachukua dakika tisa tu kupata bao la
kwanza, lililowekwa kimiani na Ibrahim Abdallah, kabla ya Mohammed Abdallah
naye kuwapatia bao la pili dakika ya 43.
Hadi filimbi ya mapumziko ya pambano hilo ya mwamuzi Ahmad
Imtehaz Heeralall wa Mauritius, Serengeti ilikuwa mbele kwa mabao hayo, huku
wakitawala mchezo na kuwafunika kabisa wenyeji hao ambao walitangulia kubezwa
na vyombo vya habari vya kwao.
Katika kipindi cha pili, Serengeti Boys waliendelea
kutawala mchezo na kufanikiwa kupata bao la tatu lililofungwa na Asad Juma Ali
katika dakika ya 50 kwa mkwaju wa adhabu ndogo 'free kick' iliyopigwa kiufundi
na kuzika rasmi matumaini ya wenyeji hao.
Serengeti Boys iliendelea kuwashambulia Shelisheli na
kufanikiwa kupata mabao matatu, hivyo kumaliza dakika 90 kwa ushindi wa
kishindo na kufuzu raundi ya pili ya michuano hiyo, ambako inaenda kuumana na
Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hii ya kuwania kufuzu
fainali za nchini Madagascar, Serengeti Boys itaanza kwa kuifuata Afrika Kusini
kati ya Agosti 5 na 7, kabla ya kurudiana jijini Dar es Salaam kati ya Agosti
19 na 21 na mshindi wa jumla kufuzu raundi ya tatu.
Fainali hizo za 11 za Afrika kwa vijana, zinatarajia
kufanyika mwakani nchini Madagascar zikihusisha nchi nane, ambazo zinatarajia
kufanyika kuanzia Aprili 2 hadi 16 mwakani, zikihusisha wachezaji waliozaliwa
kuanzia Januari Mosi, 2000.
Katika mechi ya jana, kikosi cha Serengeti kilipangwa
hivi: Ramadhani Kabwili, Israel Mwenda, Nickson Kibabage, Enrick Nkosi, Ally
Msengi, Ally Ng'anzi, Mohammed Abdallah, Shaaban Zubeir, Ibrahim Abdallah,
Rashidi Chambo na Asad Juma.
No comments:
Post a Comment