Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi ameondoka Zanzibar mchana huu kuelekea Nchini India Kupitia Mjini Dar es
salaam kwa ajili ya uchunguzi wa kawaida wa Afya yake.
Balozi Seif anatarajiwa kuweko Nchini India kwa kwa
muda mfupi na baadaye kupitia Nchini Ras Al -Khaimah kwa mapumziko mafupi pamoja
na kufanya shughuli za Kiserikali na Viongozi wa Mamlaka hiyo kabla ya kurejea nyumbani
Zanzibar kuendelea na uwajibikaji wa majukumu yake ya Kitaifa kama kawaida.
Katika safari hiyo Balozi Seif amefuatana na Mkewe
Mama Asha Suleiman Iddi baada ya kuongoza mapokezi ya mwili wa Rais Mstaafu wa
Awamu ya Pili ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mzee Aboud Jumbe Mwinyi
aliyefariki Dunia Nyumbani kwake Mji
Mwema Mjini Dar es salaam na baadaye
kwenda kutoa mkono wa pole kwa Familia ya marehemu Nyumbani kwake Migombani
Mjini Zanzibar.
Kwenye uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman
Karume Balozi Seif na Mkewe waliagwa na Mkuu wa Wilaya ya Mjini Nd. Marina Joel
Thomas akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohammed Mahmoud.
Wengine ni Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Mgeni Juma Hassan , Viongozi
Waandamizi wa Serikali, Kisiasa pamoja na Wakurugenzi na Watendaji wa Ofisi ya
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
15/8/2016.
No comments:
Post a Comment