HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 21, 2016

DRFA YAWAKUMBUSHA MAJUKUMU,KILIMANJARO QUEENS NA SERENGETI BOYS


Chama cha soka mkoa wa Dar es salaam DRFA kimezipongeza timu za taifa za soka,Kilimanjaro Queens iliyofanikiwa kuunyakua ubingwa wa michuano ya CECAFA wanawake iliyofanyika mjini Jinja nchini Uganda.

Timu hiyo iliyoiwakilisha tanzania bara na ikiwa chini ya kocha mkuu Sebastian na msaidizi wake Edina Lema,ilianza mashindano hayo kwa mafanikio makubwa na kufanikiwa kutinga katika hatua ya fainali ambapo imeisambaratisha Kenya kwa kuifunga magoli 2-1.

Mwenyekiti wa DRFA,Almas Kasongo,amesema kitendo cha Kilimanjaro Queens kutwaa kikombe hicho kinaonesha ni kwa kiasi gani walivyo tayari kwaajili ya mapambano,na endapo nguvu kubwa itatumika katika maandalizi yao wanaweza kulitangaza zaidi taifa lao.

Kasongo amelipongeza pia benchi la ufundi kwa uvumilivu mkubwa waliouonesha tangu walipokabidhiwa kikosi hicho licha ya kuwa muda na matayarisho yao hayakuwa rafiki kiushindani.

Michuano hiyo iliyoanzishwa kwa mara ya kwanza mwaka huu na baraza la vyama vya soka katika ukanda wa afrika mashariki,imeiweka tanzania katika ramani kupitia medani ya mpira wa miguu barani afrika.

Mbali na timu hiyo ya wanawake, Drfa imeimwagia sifa Serengeti Boys inayosaka tiketi ya kutinga katika michuano ya kuwania kombe la mataifa ya afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 itakayofanyika mwezi april nchini Madagascar.

Kikosi hicho chini ya kocha Bakari Shime, kimesaliwa na mchezo mmoja wa marudiano dhidi ya Congo Brazzaville kabla ya kutinga katika fainali hizo,ambapo katika mchezo wa kwanza wamefanikiwa kupata ushindi wa magoli 3-2.

Mwenyekiti Kasongo ameongeza kuwa mafanikio ya vikosi hivyo vya taifa ni ya watanzania wote na kuwaomba wachezaji wasibweteke na hali hiyo na badala yake wazidi kujituma ili kuboresha viwango vyao vya kucheza soka na kulisaidia taifa.

IMETOLEWA NA CHAMA CHA SOKA MKOA WA DAR ES SALAAM,DRFA

No comments:

Post a Comment

Pages