HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 22, 2016

TAASISI ZACHANGIA SH. MIL.172 MAAFA KAGERA

  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea hundi ya shilingi milioni 20 kutoka kwa Meneja wa Kanda wa LAPF, Amina Kassim (kulia) na  Kafiti Kafiti wa LAPF  ukiwa ni mchango wa Mfuko huo  kwa waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera. Makabidhiano hayo  yalifanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dar es salaam Septemba 22, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)



xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx


TAASISI sita zikiwemo za dini na kijamii zimechanga jumla ya sh. milioni 172.5 zikiwa ni misaada kwa wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera Septemba 10, mwaka huu.

Mchango huo umepokelea leo jioni (Alhamisi, Septemba 22, 2016) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam.
Akikabidhi hundi kwa Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, Bw. Ian Ferrao alisema kiasi cha sh. Milioni 100 kimekusanywa kutoka kwenye mfuko wa Vodacom Foundation pamoja na wadau wao.

Bw. Ferrao amesema kampuni ya Vodacom imekuwa mstari wa mbele kusaidiana na Serikali katika uboreshaji wa miradi mbalimbali za kijamii.....

Taasisi nyingine iliyochangia ni Mfuko wa Pensheni wa LAPF  ambapo Meneja wa Kaya ya Dar es Salaam, Amina Kassim amemkabidhi Waziri Mkuu hundi ya sh. milioni 20.
Pia Jumuiya ya Kiislam Ahmadiyya imekabidhi msaada wa sh. milioni 10 kati ya hizo sh. milioni nne ni fedha taslimu na zilizobaki ni mabati na mifuko ya saruji.

Naye Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya Advent, Dhruv Jog amemkabidhi Waziri Mkuu msaada wa tani 40 za saruji yenye thamani ya sh. milioni 16.5 na kusema  kwamba wameshtushwa na tukio hilo na tayari saruji hiyo imeanza kupelekwa Kagera.

Kwa upande wake mwakilishi wa Taasisi ya kimataifa ya Art of Living, Neetu Kulshreshtha wametoa msaada wa vyakula mbalimbali pamoja dawa vikiwa na thamani ya sh. milioni 10.
Dk. Ave Maria Semakafu amemkabidhi Waziri Mkuu hundi ya sh milioni 16 kwa niaba ya makundi mawili ya mtandao wa kijamii wa WhatsApp. Makundi hayo yanaitwa Leaders na Uongozi.

Akitoa shukrani kwa waliotoa michango yote hiyo, Waziri Mkuu amewashukuru kwa misaada hiyo na kuahidi kuwa Serikali itahakikisha michango hiyo inafikishwa Kagera kwa walengwa.
“Tunashukuru sana kwa michango yote. Tunashukuru na makundi ya WhatsApp ya Leaders na Uongozi ambayo nayo yameamua kuja kutuchangia. Michango hii inaonyesha kuguswa na mapenzi ya dhati kwa waliopatwa na maafa,” amesema. 

Waziri Mkuu amesema Serikali inakamilisha tathmini ya maafa hayo na kuahidi kutoa taarifa ya kiasi kilichokusanywa na kiasi kilichotumika. Amewaomba wananchi waliotoa ahadi zao za michango wakamilishe ahadi zao.

Akaunti ya maafa imefunguliwa katika Benki ya CRDB yenye Namba. 015 222 561 7300 kwa jina la KAMATI MAAFA KAGERA – Swiftcode: CORUtztz na namba za simu za mkononi zinazotumika kupokea michango hiyo ni 0768-196-669 (M-Pesa), au 0682-950-009 (Airtel Money) au 0718-069-616 (Tigo Pesa).
Tetemeko hilo lililotokea Jumamosi, Septemba 10, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 17 na wengine 440 walijeruhiwa kati yao watu 253 walifikishwa Hospitali ya Mkoa, 153 walilazwa, 113 walitibiwa na kuruhusiwa na wengine 38 wanaendelea na matibabu ambapo kati yao watu 23 wamefanyiwa upasuaji mkubwa na wanaendelea vizuri. 

Pia tetemeko hilo limesababisha nyumba 2,063 kuanguka huku nyingine 14,081 zikiwa katika hali hatarishi baada ya kupata nyufa na 9,471 zimepata uharibifu mdogo huku wananchi 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S.  L. P. 3021,
11410 - DAR ES SALAAM.
ALHAMIS, SEPTEMBA 22, 2016.

No comments:

Post a Comment

Pages