HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 11, 2016

WAZIRI MKUU AONGOZA WANANCHI KUAGA MIILI YA WALIOKUFA KWA TETEMEKO

Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa akitoa heshima za mwisho kwa marehemu walipoteza maisha kutokana na tetemeko la ardhi  mkoani kagera katika ibada maalum ya kuwaombea marehemu hao iliyofanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba jana.  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Baadhi ya majeneza ya marehemu waliokufa kwa tetemeko la ardhi yakiwa katika Uwanja wa Kaitaba wakati wa ibada maalum ya kuwaombea. (Picha na Ashura Jumapili)
Waziri Mkuu akimjulia hali mmoja wa majeruhi wa tetemeko la ardhi alipofika kuwapa pole na kuwafariji katika hospitali ya Mkoa wa Kagera. (Picha na Ashura Jumapili)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananfunzi wa Shule ya Sekondari ya Nyakato mkoani Kagera wakati alipokwenda  shuleni hapo Septemba 11, 2016 kujionea athari za tetemeko la ardhi lililoukumba mkoa huo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameongoza maelfu ya wananchi wa Manispaa ya Bukoba mjini kuaaga miili ya watu 16 waliofariki kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea jana (Jumamosi, 10 Septemba, 2016 mkoani Kagera.

Tetemeko hilo lilitokea jana Alasiri limesababisha vifo vya watu 16 na wengine 253 kujeruhiwa. Pia limesababisha maelfu ya wananchi kukosa makazi baada ya nyumba 840 kuanguka na nyingine 1264 zikipata nyufa yakiwemo majengo 44 ya taasisi mbalimbali za umma.

Kufuatia tukio hilo Waziri Mkuu ambaye alimuwakilisha Mheshimiwa Rais, Dk. John Magufuli amewaomba wananchi kuwa watulivu wakati Serikali ikiendelea kufanya tathmini ya athari zilizotokana na maafa hayo.

“Poleni sana tukio hili ni kubwa na halijawahi kutokea nchini. Haya yote ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Tuendelee kuwa na imani na watulivu  Serikali ipo pamoja nanyi na haitawatupa mkono,” amesema.

Waziri Mkuu amesema Kamati ya Maafa ambayo ipo katika Ofisi ya Waziri ya Mkuu itakwenda wilaya za Kyerwa, Karagwe na Bukoba mjini kwa ajili ya kufanya tathmini na kubaini athari zilizosababishwa na tetemeko hilo na kuona namna ya kuwasaidia waathirika.

Wakati huo huo Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wa mkoa huo kuchukua hatua za haraka kwa kuwatafutia eneo salama la kulala wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyakato ambayo mabweni yake yote yameathirika na tetemeko hilo na hayafai kutumika.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo baada ya kutembelea shule hiyo na kujionea namna mabweni ya shule hiyo yalivyopata nyufa hali iliyosababisha wanafunzi kulala uwanjani.

Pia Waziri Mkuu ameiagiza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuangalia kama kuna tetemeko linguine linaweza kutokea nchini ili Serikali iweze kuchukua tahadhari pamoja na kutoa elimu kwa umma namna ya kujikinga.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu amesema kwa sasa wanaendelea na jukumu la kuwatafutia makazi wananchi ambao nyumba zao zimeanguka. Pia mkoa unaendelea kufanya tathmini ya kina kujua athari zilizosababishwa na tetemeko hilo.

Awali Waziri Mkuu alitembelea Hospitali ya Mkoa wa Kagera ambako majeruhi 170 wamelazwa na kutoa pole na kwamba anawaombea kwa Mwenyezi Mungu wapone haraka na wenye matatizo ambayo yanahitaji matibabu kwenye hoispitali kubwa Serikali itahakikisha wanapelekwa huko na kuhudumiwa.

 IMETOLEWA NA:              
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI,SEPTEMBA 11, 2016

No comments:

Post a Comment

Pages