HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 31, 2016

BODI YA MIKOPO KUHAKIKI MIKOPO YA WANAFUNZI

Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Abdul Razaq Badru akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusu vigezo vya utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2016/17. (Picha na Francis Dande)

NA ZAWADI CHOGOGWE
BODI  ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), imesema kuanzia sasa  itaanza  kuhakiki  taarifa  za wanufaika wote  wa mikopo  wanaoendelea na  masomo, huku watakaobainika kukosa vigezo watarejesha  kiasi cha fedha ambacho tayari wameshapokea.
Kauli  hiyo ilitolewa jana Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Bodi hiyo, Abdul Badru,  wakati akizungumza na wandishi wahabari  alipokuwa akitaja  vigezo vya utoaji wa mikopo kwa mwaka  wa masomo   wa  2016/17.
Badru  alisema vigezo  ambavyo viliwekwa na Serikali na kutangazwa kwa waombaji  vinazingatia  wanafunzi ambao ni yatima, walemavu, wanaotoka  katika familia zenye hali duni ya kimaisha hususa waliosoma katika shule za umma na vipaumbele vya kitaifa.
Alisema vipaumbele vya kitaifa  ni vile  vinavyoendana na mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano, Dira ya Taifa ya Maendeleo  2025 na mafunzo ambayo   yatazalisha wataalam wanaokidhi mahitaji ya kitaifa katika fani za mbalimbali.
Alitaja fani hizo  kuwa ni  Sayansi  za tiba na Afya, Ualimu wa Sayansi na Hisabati, Uhandisi wa Viwanda, Kilimo, Mifugo, Mafuta na Gesi Asilia, Sayansi asilia na Sayansi za Ardhi, Usanifu Majengo na Miundombinu.
Badru alisema kwa upangaji wa mikopo kwa mwaka 2016 hadi 2017 umezingatia bajeti ya Sh. Bilioni  483 ili yopitishwa na Bunge kwa ajili ya kuwakopesha jumla ya wanafunzi 119, 012.
Alisema kati yao, wanafunzi  25,717 ni wale wa mwaka wa kwanza na wanafunzi  93,295 ni wale wanaendelea katika taasisi mbalimbali nchini.
“Baada ya uchambuzi wa maombi ya mikopo kuka milika, jumla  ya waombaji  20,391 wamepangiwa mikopo katika awamu ya kwanza ambayo imekamilika na orodha zenye majina ya wanufaika hao zimetumwa kwa vyuo walivyopangiwa na Tume ya Vyuo  Vikuu Tanzania(TCU),”alisema Badru.
Badru alisema waombaji  27, 053  hawakujumuishwa katika uchujaji na upangiwaji wa mikopo kwa mujibu wa vigezo.
“Baada ya  Uchujaji huu, idadi ya waombaji wenye sifa stahiki ilipungua hadi  30,957 ambao waliingizwa kwenye mfumo wa kuchakata na kupanga mikopo kwa mujibu wa sifa zao na vigezo vilivyowekwa,”alisema Badru.
Alisema  baada ya kukamilisha upangaji  na utoaji mikopo kwa awamu ya kwanza  yenye wanafunzi 20,391 wa mwaka wa kwanza, bodi inaandaa awamu ya pili ya upangaji mikopo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza ili kukamilisha lengo la kutoa mikopo kwa wanafunzi 25,717 wa mwaka wa kwanza kwa mwaka huu 2016 hadi 2017.
“Asilimia 90 pesa ya wanafunzi wapya na wanaoendelea zimeshapelekwa kwenye akaunti za vyuo vyao na taasisi zinazohusika,”alisema  Badru.
Katika hatua nyingine, Badru alisema  kuanzia kesho watafungua dirisha la rufaa la waombaji ambao hawakuridhika  na matokeo ya upangaji wa awamu ya kwanza na kwamba zoezi hilo litakamilika baada ya siku 90.
Kwa  upande  wake, Rais wa Serikali ya  wanafunzi  wa  Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Kilonzo Mringo alisema mpaka sasa zaidi ya wanafunzi  50 bado hawajapewa mikopo.
“Serikali  ikae chini ili angalie  suala hili  kwa umakini  ili  wanafunzi  wote wenye sifa  za kupewa mikopo wapatiwe mikopo hiyo,”alisisitiza Mringo.

No comments:

Post a Comment

Pages