Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimshukuru mbunge wa Viti
Maluum CCM Mkoa wa Lindi, Amida Abdalah baada ya kuchangia mabati mia moja kwa ajili
ya ujenzi wa wodi ya wazazi katika Hospitali ya wilaya ya Ruangwa. Katikati ni Mama Majaliwa
na kulia ni Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Dk. Japhet Simeo makabidhiano hayo
yamefanyika katika Hospitali Ruangwa. (Picha na Chris Mfinanga)
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea msaada wa mabati 100 yenye thamani ya zaidi ya sh. milioni mbili kutoka kwa Mbunge wa Viti maalum mkoa wa Lindi Mhe. Hamida Abdallah.
Msaada huo umetolewa leo (Jumatano, Oktoba 19, 2016) katika hospitali ya wilaya ya Ruangwa wakati wa ziara ya Waziri Mkuu hospitalini hapo.
Mbunge huyo amesema amekabidhi msaada huo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa mwezi Aprili mwaka huu wakati Waziri Mkuu alipofanya ziara katika Hospitali hiyo.
“Ulipofanya ziara ya mwezi wanne hospitalini hapa nilikuahidi kukupa mabati 100 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya wanawake. Nilitoa ahadi hii baada ya kuona jitihada kubwa unazozifanya katika kuimarisha hospitali hii,” amesema.
Akipokea msaada huo Waziri Mkuu amemshukuru Mhe. Hamida kwa kutekeleza ahadi yake na kumuomba aendelee kuisaidia hospitali hiyo pindi anapopata nafasi.” Nashukuru sana kwa msaada wako tunajua kutoa ni moyo na si utajiri,”.
Wakati huo huo Waziri Mkuu amesema mkakati wake kwa sasa ni kuboresha huduma za afya kwa kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na zahanati ili kuwawezesha wananchi kupata matibabu karibu na makazi yao.
“Nataka sekta ya afya inapata mafanikio makubwa. Nitashirikiana na wananchi kuhakikisha kunakuwa na zahanati katika kila kijiji na vituo vya afya kwenye kata zote,” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Bw. Andrea Chezue alimshukuru Waziri Mkuu kwa jitihada zake za kuboresha huduma hospitalini hapo.
Amesema hivi karibuni walipokea sh. milioni 100 kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Lindi kwa ajili ya ukarabati wa wodi mbili ambazo tayari ukarabati huo umekamilika na zitaanza kutumika kuanzia Novemba 15 mwaka huu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, OKTOBA 19, 2016
No comments:
Post a Comment